Juhudi za kupunguza uhaba wa madawati na vifaa vya kujifunzia katika Wilaya za Kondoa na Chemba, mkoani Dodoma, zimepata msukumo baada ya Benki ya NMB kukabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh47.6 milioni kwa shule nane za msingi na sekondari.

Vifaa hivyo ni madawati, viti, meza, vitanda vya ghorofa na magodoro. Akipokea msaada huo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kwadero, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatuma Nyangasa, alisema utaboresha mazingira ya kujifunzia. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Hassan Mnyika, alisema baadhi ya shule bado zina uhaba wa madawati unaowalazimisha wanafunzi kukaa chini.

Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Janeth Shango, alisema elimu ni miongoni mwa maeneo yanayoungwa mkono na benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali. Alisema NMB itaendelea kusaidia kupunguza changamoto za vifaa na kuboresha mazingira ya kujifunzia kulingana na mahitaji ya shule nchini.

Shule zilizonufaika ni Chemba, Mondo na Soya wilayani Chemba, na Mnenia, Kitewo, Deli, Kwadero na Bolisa wilayani Kondoa. Sekondari ya Wasichana Kwadero imepata pia vitanda 15 vya ghorofa na magodoro, huku msaada huo ukitarajiwa kupunguza uhaba na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi shuleni.