Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amewataka wahitimu wa Mahafali ya 63 ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, Mwanza ambao wamehitimu Kozi ya Uhifadhi
wa Wanyamapori, Himasheria, Uongozaji Watalii na Usalama ambao jumla yao ni 388, kuzingatia maadili, weledi na uwajibikaji wanapoingia katika utumishi wa umma.
Dkt. Abbasi alikuwa Mgeni Rasmi katika mahafali hayo Septemba 17, 2026, ambapo amewapongeza wahitimu kwa kuonesha ukakamavu na uelewa mkubwa wa masomo yao, akibainisha kuwa wamejiandaa vyema katika jukumu la kulinda rasilimali za wanyamapori na kukabiliana na uhalifu dhidi ya wanyamapori.
“Mnapoingia kazini, zingatieni maadili na mfanye kazi kwa weledi,” amesisitiza Dkt. Abbasi.
Katika hotuba yake, Dkt. Abbasi pia amechukua hatua kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo kwa kuwezesha upatikanaji wa vitabu, darubini 200 kwa ajili ya mafunzo, ndege nyuki mbili za mafunzo ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu, mahema zaidi ya 20 pamoja na buti 50 kwa ajili ya askari.
Aidha, ameahidi kuwezesha ujenzi wa madarasa ya kisasa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi amesema Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Samia Scholarship, itatoa fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watakaofika kusoma katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.

Hatua hizo zinaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mafunzo ya wataalamu wa wanyamapori na kuwaandaa watumishi wenye weledi, nidhamu na uwezo wa kulinda urithi wa asili wa Tanzania.
