Morogoro, 16 Septemba 2026
Tanzania imezindua rasmi programu ya WISER ActionFirst™ inayolenga kuimarisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kuchukua hatua za mapema, hususan katika sekta za kilimo na mifugo, ili kupunguza athari za majanga yanayohusiana na hali ya hewa na tabianchi.
Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa CATE Hotel, Morogoro, ukiambatana na Warsha ya Kitaifa ya Ushirikishwaji wa Wadau katika Kuandaa Taarifa Mahususi za Hali ya Hewa kwa Sekta za Kilimo na Mifugo, inayofanyika tarehe 16–18 Septemba 2026.
Akizindua rasmi programu hiyo na kufungua warsha, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Brigedia Jenerali Hosea Maloda Ndagala, alisema Tanzania inalenga kuimarisha mfumo wa tahadhari za mapema unaowezesha wananchi na taasisi kuchukua hatua kabla ya majanga kutokea.
Alisema kutoa utabiri pekee hakutoshi, bali kuna haja ya kueleza nini kifanyike. “Tunapaswa kutoka katika mfumo unaotuambia hali ya hewa inayotarajiwa kuwa vipi, kwenda kwenye mfumo unaotueleza hali hiyo inamaanisha nini, nini kifanyike, nani afanye, wapi na lini.”
Brigedia Jenerali Ndagala alisema kilimo na mifugo ni miongoni mwa sekta zilizo katika hatari kubwa kutokana na mafuriko, vipindi virefu vya ukavu, joto kali, upepo mkali, pamoja na wadudu na magonjwa yanayoathiriwa na hali hivyo, hatua za mapema zina umuhimu mkubwa katika kulinda uzalishaji, usalama wa chakula, maisha na mali, huku zikisaidia kupunguza gharama za kukabiliana na majanga baada ya kutokea.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Ofisi ya WMO Kanda ya Afrika, Dkt. Agnes Kijazi, alisema tukio hilo ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kuimarisha Utabiri Unaozingatia Hatua za kuchuka (Action-Based Forecasting – ABF).
Dkt. Kijazi alisisitiza, mchakato wa uandaaji shirikishi wa taarifa unalenga kuziba pengo kati ya taarifa za utabiri na hatua za mapema kwa kuimarisha ushirikiano kati ya huduma za hali ya hewa, huduma za kisekta, taasisi za menejimenti ya maafa, wadau wa maendeleo, wizara, vyombo vya habari na jamii zilizo katika hatari.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Geofrid Chikojo (Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora-TMA), alisema WISER ActionFirst™ itasaidia kuongeza matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta za kilimo na mifugo.
Alisema TMA tayari inatoa Utabiri Unaozingatia Athari (Impact-Based Forecasting – IBF) kwa sekta mbalimbali, na mpango wa ActionFirst™ utasaidia kuendeleza msingi huo kwa kuhusisha watumiaji wa taarifa katika kuandaa taarifa zinazokidhi mahitaji yao.
“Ushirikishwaji wa wadau utasaidia kuboresha taarifa za tahadhari za mapema zinazolenga mahitaji ya sekta za kilimo na mifugo na kuongeza matumizi yake katika kufanya maamuzi”.Alisisitiza Dkt. Chikojo
Kwa upande wake, Mwakilishi wa WISER na UK Met Office, Bw. John Mungai, alifafanua kuwa ActionFirst™ inalenga kuhamisha mtazamo kutoka kwenye swali la “hali ya hewa itakuwaje?” kwenda kwenye maswali ya “hali hiyo ya hewa itafanya nini?” na “nini kinapaswa kufanyika?”
Programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Menejimenti ya Maafa, pamoja na Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Taasisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UK Met Office) na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

