……..

NA DENIS MLOWE, IRINGA

WANANCHI wa Kata ya Mkwawa katika Jimbo la Iringa Mjini wamemweleza Mbunge wao, Fadhili Ngajilo, changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao, zikiwamo za vivuko, barabara, majitaka, matuta, ukosefu wa fursa kwa vijana na uhitaji wa kukamilishwa kwa baadhi ya miradi ya kijamii.

Changamoto hizo ziliwasilishwa mbele ya mbunge huyo katika mkutano wa wananchi uliofanyika Mtaa wa Bwawani, Kitongoji cha Don Bosco B, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukutana na wananchi katika kata mbalimbali za Jimbo la Iringa Mjini.

Akizungumza katika mkutano huo, mkazi wa Don Bosco, Kasimu Muhanga, alisema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya vivuko katika maeneo mbalimbali, hali inayosababisha ugumu wa kuvuka hasa wakati wa mvua.

Muhanga alisema baadhi ya vivuko vilivyopo vinahitaji kufanyiwa kazi ili viweze kutoa huduma salama kwa wananchi, huku akiomba Mbunge Ngajilo kusaidia kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa eneo hilo, Fedayini Malangalila, alisema moja ya changamoto kubwa inayowakabili vijana ni upatikanaji wa fursa za kiuchumi na ajira.

Alisema pamoja na kuwepo kwa programu na vikundi mbalimbali vinavyolenga kuwawezesha vijana, baadhi ya wananchi bado hawajafahamu kwa uwazi namna ya kunufaika na fursa hizo.

Aidha, wananchi waliiomba Serikali kuangalia hali ya barabara katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo, wakieleza kuwa mvua kubwa imekuwa ikisababisha uharibifu wa miundombinu, ikiwamo misingi ya barabara na maeneo ya kupitisha maji.

Akijibu hoja hizo, Ngajilo alisema ziara yake katika Kata ya Mkwawa ni sehemu ya mpango wake wa kutembelea kata zote za Jimbo la Iringa Mjini ili kukutana moja kwa moja na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kupata pia mrejesho kuhusu maendeleo yaliyofanyika.

Alisema hoja zinazotolewa na wananchi ni muhimu kwa sababu zinampa nafasi ya kuzifikisha katika ngazi mbalimbali za Serikali na kuzifuatilia hadi zipate majibu.

“Nimekuja hapa kwa sababu nataka kusikia kero zenu, lakini pia nataka kusikia furaha zenu. Kila jambo mtakalolieleza hapa tutalipokea na tutalifanyia kazi,” alisema Ngajilo.

Akizungumzia changamoto ya barabara, Ngajilo alisema amekuwa akifuatilia suala la uboreshaji wa barabara kutoka Iringa Mjini kuelekea maeneo ya Itamba, Mgera, Hoho na Mkwawa.

Alisema juhudi zimeanza kuchukuliwa na Serikali katika ujenzi wa baadhi ya vipande vya barabara hiyo, akieleza kuwa sehemu ya ujenzi imeanza kutoka Pawaga kuelekea upande wa Itamba.
Ngajilo alisema ujenzi huo unahusisha kipande cha takribani kilomita 20 kinachoendelea kujengwa, huku hatua zikitarajiwa kuendelea katika maeneo mengine kulingana na utekelezaji wa mradi.
Alisema nafasi yake kama Mbunge ni kuwa sauti ya wananchi ndani ya Bunge na katika majadiliano na Serikali, hivyo taarifa na hoja zinazotoka kwa wananchi ni msingi wa kufuatilia utekelezaji wa mahitaji yao.

“Niwaseme wazi kwamba sauti hii ni ya kwenu. Kile ninachokisema lazima kitoke kwenu. Diwani akisema, anasema ya kwenu; mbunge akisema, anasema ya kwenu,” alisema.

Ngajilo alisema ataendelea kushirikiana na viongozi wa Kata ya Mkwawa na wananchi katika kufuatilia kero zilizowasilishwa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushiriki katika maendeleo ya maeneo yao.

Mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya Mbunge Ngajilo wa kata kwa kata katika Jimbo la Iringa Mjini, yenye lengo la kusikiliza wananchi, kutathmini changamoto za maeneo yao na kueleza hatua zinazochukuliwa katika kuzitatua.
Awali, Diwani wa Kata ya Mkwawa, Amri Kalinga, alisema Serikali za mitaa kwa kushirikiana na Mbunge Ngajilo zimekuwa zikifuatilia changamoto mbalimbali za wananchi, ikiwamo tatizo la majitaka.

Kalinga alisema kuna mpango wa kuondoa miundombinu ya majitaka katika baadhi ya maeneo ya Don Bosco na kuielekeza katika maeneo yatakayofaa zaidi, ili kupunguza athari kwa wananchi.

Kalinga pia alizungumzia ujenzi wa kivuko katika eneo la Don Bosco, akisema fedha za Mfuko wa Jimbo ziliwahi kuelekezwa kupitia Manispaa ya Iringa kwa ajili ya ujenzi wa kivuko hicho.

Aidha, alitaja uwepo wa matuta kuwa suala linalohitaji kuangaliwa kutokana na kasi ya magari, pikipiki na bajaji katika baadhi ya barabara za eneo hilo.