Picha,Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Likuyumandela akiwa katika ziara ya kusikikiza kero ya Wananchi wa Jimbo hilo. 

…………. 

Na Mwandishi Wetu,

Namtumbo

MBUNGE wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera,ameiomba Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kuongeza nguvu katika kudhibiti wanyamapori wanaotoka kwenye hifadhi na kwenda kwenye makazi ya wananchi kula mazao na kufanya uharibufu.

Ametoa ombi hilo baada ya wananchi wa  kijiji cha Likuyumandela wilayani Namtumbo kulalamikia wanyama hao.

Dkt Homera ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria alisema,wanyamapori hususani tembo wamekuwa tishio  kwa usalama wa wananchi na mali zao,hivyo hatua za haraka zinahitajika  dhidi ya wanyama hao ambao  wanahatarisha maisha ya wananchi na mali zao.

 Waziri Homera alisema  kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili  wananchi ikiwemo ukosefu wa majisafi na salama,umeme na kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Alisema,miongoni mwa barabara  inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami ni Mtonya-Likuyu ambayo  tayari imewekwa kwenye mpango wa Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia ujenzi WA Barabara huyo na itakapojengwa  itatoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Naye Mhifadhi  Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere Kanda ya Kusini Deogratius Ndelolia alisema,mgongano kati ya binadamu na wanyamapori unaendelea kufanyiwa kazi na Tanapa inatumia vituo vya askari,magari,pikipiki na ndege nyuki katika kudhibiti.

“Sasa tuna kituo kimoja cha askari katika kijiji cha Nambecha na kituo cha muda katika kijiji cha Likuyuseka,hata hivyo nitawasilisha  ombi la kuongeza vituo katika kijiji cha Mchomoro,Likuyu na Ligera”alisema.

Alisema,eneo la Selou lilikuwa pori la akiba kabla ya mwaka 2019 kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kwa sasa limegawanywa huku Tanapa ikiendelea na jukumu la kuhifadhi  rasilimali za misitu na wanyama zilizopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Nyerere pamoja na vyanzo vya maji.

Ndolelia alieleza kuwa,wanyama wamegundua maeneo salama ya kuishi na kuzaliana na wakati mwingine hukaribia na kufika kwenye makazi ya  wananchi, hata hivyo Serikali inaendelea na mikakati ya kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Mkazi wa kijiji hicho Joackim James alisema,changamoto ya wanyamapori hususani fisi na tembo ni kubwa kutokana na kuingia kwenye mashamba na kufanya uharibu.

Alisema,wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao  ambapo ameiomba Serikali kuimarisa udhibiti wa wanyama katika barabara ya Likuyu-Mandela  kwani wananchi hukutana na wanyama hao mara kwa mara.