Na Farida Said KATESHI, MANYARA

. Mamia ya watalii wa ndani walijitokeza Septemba 12–13, 2026 kushiriki Mount Hanang’ Nyama Choma Festival, lililofanyika kwa mara ya sita katika Msitu wa Mazingira Asilia wa Mlima Hanang’.

Tamasha hilo liliwakutanisha wananchi na wageni kwa mchanganyiko wa burudani na utalii wa mazingira, huku washiriki wakipata fursa ya kufurahia nyama choma, kufanya hiking, kupiga kambi na kujionea vivutio mbalimbali vya asili.

Miongoni mwa vivutio vilivyowavutia washiriki ni maporomoko ya maji, ndege wa aina mbalimbali na wanyama, pamoja na mandhari ya Mlima Hanang’ na utajiri wa ikolojia unaopatikana katika msitu huo.

Mmoja wa washiriki, Raphael Joel, amesema kuendelea kwa tamasha hilo kunachochea hamasa kwa Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

“Matamasha kama haya yanaongeza hamasa kwa watalii wa ndani kutembelea vivutio vilivyopo nchini. Tunapata burudani, lakini pia tunajifunza umuhimu wa kuhifadhi mazingira,” amesema Joel.

Ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kutumia matukio kama hayo kutangaza utalii wa ndani na kuhamasisha wananchi kuthamini na kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.

Mhifadhi Mkuu wa Msitu wa Mazingira Asilia wa Mlima Hanang’, Abubakar Mpapa, amesema tamasha hilo linatoa fursa kwa wageni kufurahia nyama choma, kupiga kambi na kujionea vivutio vya asili vilivyopo katika eneo hilo.

Amesema TFS itaendelea kuhamasisha utalii wa ndani kupitia matukio mbalimbali, huku ikisisitiza matumizi endelevu ya misitu na ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa mazingira.