DODOMA RS

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka viongozi wa dini kutumia ushawishi na imani kubwa waliyonayo katika jamii kuimarisha maadili mema, kulinda amani na kudumisha umoja wa kitaifa.

Mhe. Senyamule ametoa wito huo  Septemba 13, 2026, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Wachungaji wa makanisa yaliyo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema viongozi wa dini wana nafasi ya kimkakati katika kujenga jamii yenye maadili, kutokana na kiwango kikubwa cha imani na heshima wanachopewa na wananchi wanaowaongoza kiroho.

“Viongozi wa dini mna nafasi kubwa katika kujenga maadili mema, kudumisha amani na kuimarisha umoja wa kitaifa. Mnaaminika sana na wananchi, pengine kuliko watu wengine wengi. Hivyo, mafundisho na matendo yenu yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Mhe. Senyamule.

Amewataka viongozi hao kuendelea kusimamia misingi ya haki, upendo, msamaha na uwajibikaji, huku wakiwa chanzo cha faraja kwa wenye huzuni, matumaini kwa waliokata tamaa na msaada kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa malezi bora ya kiroho na kimaadili, hususan kwa watoto na vijana, akieleza kuwa viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kutoa mafundisho na mwongozo unaochangia ustawi wa kiroho, kijamii na kiuchumi wa wananchi.

Mhe. Senyamule pia amewataka viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa malengo ya Dira hiyo yanaweza kufikiwa kupitia dhamira, ushirikiano na ushiriki wa pamoja wa wananchi.

Amesisitiza pia umuhimu wa viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira 2050, akibainisha kuwa Dira hiyo inatoa fursa kwa Watanzania mmoja mmoja, makundi mbalimbali na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa, amesema viongozi wa dini wameitwa na kukabidhiwa jukumu la kuwahudumia na kuwaongoza kundi la waumini wa Mungu kwa unyenyekevu.

Dkt. Malasusa amesisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kutekeleza kwa uaminifu wito wao, huku wakimtegemea Mungu kama chanzo cha nguvu na uwezo wa kutimiza majukumu waliyopewa.

Mkutano huo wa siku tano unatoa fursa kwa wachungaji kushiriki katika maombi, kupata maarifa kuhusu masuala mbalimbali, kubadilishana uzoefu na kuimarishana katika wito wao wa kulitumikia Kanisa, jamii na Taifa.

Mkutano huo unaongozwa na ujumbe unaopatikana katika Nehemia 2:20, unaosema: “Mungu wa mbinguni, ndiye atakayetufanikisha.” Ujumbe huo unalenga kuwatia moyo na kuwaimarisha wachungaji katika kutekeleza wito wao wa kiungu, kwa imani kwamba Mungu aliyewakabidhi jukumu hilo atawawezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa.