Wananchi wa Kata ya Dimani, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani, wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwapatia mitungi ya gesi ya kupikia kwa bei nafuu, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Akizungumza baada ya kupokea mitungi hiyo, Diwani wa Kata ya Dimani, Bw. Yusuph Binda, amesema wananchi wamekuwa wakitumia zaidi kuni na mkaa katika shughuli za kupikia, hali iliyowasababishia changamoto mbalimbali, ikiwemo moshi, uchafuzi wa mazingira na athari za kiafya.
Amesema kupatikana kwa mitungi hiyo kumewapa wananchi fursa ya kuanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameweza kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kama mama, tumeona huruma yako, na sisi leo tunaahidi kuhakikisha wananchi wanatumia nishati hii kwa usahihi na usalama,” alisema.
Bw. Binda ameahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi na salama ya gesi kupitia mikutano na makongamano mbalimbali, ili kuhakikisha nishati hiyo inatumika kwa usalama na kuleta tija kwa familia na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka REA, Bi. Jaina Msuya, amewahimiza wananchi kuweka akiba kidogo kidogo kwa ajili ya kujaza mitungi ya gesi mara itakapomalizika, ili kuhakikisha matumizi ya nishati hiyo yanaendelea kuwa endelevu.
Amesema, kwa mfano, endapo gharama ya kujaza mtungi ni Shilingi 26,000, mtumiaji anaweza kuweka akiba kila anapotumia gesi, kwa kiasi kidogo kulingana na uwezo wake, ili ifikapo wakati wa kujaza mtungi awe amekusanya fedha za kutosha.
Wananchi walipata mitungi ya gesi hiyo wamesema itawasaidia kupunguza muda wa kupika, kuondoa usumbufu wa kutafuta kuni na kupunguza athari za moshi unaotokana na matumizi ya kuni.
Mmoja wa wananchi hao amesema matumizi ya kuni yalikuwa yakimlazimu kukabiliana na moshi wakati wa kupika, hali iliyokuwa ikisababisha macho kutoa machozi na wakati mwingine kuungua kutokana na cheche za moto.
“Changamoto niliyokuwa napitia kutumia kuni ilikuwa moshi. Wakati tunapopika tunatoa machozi, na mwisho wake tunaweza kupata madhara kwenye macho. Sasa tunataka majumbani kwetu tusizione kuni, tutumie gesi,” alisema.

