Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka viongozi na taasisi za Serikali kuongeza utoaji wa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu hali ya El Niño na mvua kubwa zinazotarajiwa, ili hatua za kujikinga na kupunguza madhara zichukuliwe mapema.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 11 Septemba 2026, baada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Masjid Swafaa, Gongoni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema wananchi wanapaswa kufuatilia kwa karibu taarifa na maelekezo yatakayotolewa na Serikali pamoja na mamlaka husika kuhusu mwenendo wa mvua, na kuchukua tahadhari mapema ili kupunguza madhara na usumbufu unaoweza kujitokeza.

Rais Dkt. Mwinyi amewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema, hususan kwa kuepuka maeneo ya mabondeni, mikondo na njia za maji, pamoja na kuhama maeneo yenye hatari pale itakapohitajika, huku akisisitiza umuhimu wa kumuomba Mwenyezi Mungu kwa dua sambamba na kuzingatia maelekezo yatakayotolewa na mamlaka husika.

Aidha, amesema Serikali kupitia vikosi na taasisi zake inaendelea na maandalizi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na El Niño na mvua kubwa, ikiwemo kuweka utaratibu wa kutoa msaada kwa wananchi watakaoathirika na kuimarisha uwezo wa uokozi pale itakapohitajika.

Rais Dkt. Mwinyi pia amezitaka Manispaa zote za Unguja na Pemba kuhakikisha mifereji, mikondo na njia za kupitisha maji zinasafishwa, ili kupunguza uwezekano wa maji kutuama na madhara ya mafuriko katika maeneo mbalimbali.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya maandalizi yanayoendelea kufanywa na Serikali kwa lengo la kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka husika na kuzingatia taarifa na maelekezo rasmi yatakayotolewa.

Kuhusu upatikanaji wa huduma muhimu, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imejiandaa kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata mahitaji ya msingi katika kipindi hicho, ikiwemo chakula na huduma za afya, pamoja na kuhakikisha bohari za dawa zina akiba ya kutosha

Amesisitiza kuwa taasisi na mamlaka zote zinazohusika zinapaswa kuwa katika hali ya utayari wakati wote ili huduma na msaada unaohitajika utolewe kwa wananchi kwa wakati endapo changamoto zitajitokeza.