Na WMJJWM – Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ni nguzo ya kuleta mageuzi ya kifikra na kuchochea maendeleo endelevu ya kijamii.
Maswi ameyasema hayo Septemba 09, 2026, Jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha watumishi wa Wizara hiyo kinacholenga kujenga uelewa wa pamoja kwa watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii.
Maswi amewataka watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na dhamira moja ya kuwahudumia wananchi na kutatua changamoto zao, akihimiza ushirikiano, kubadilishana taarifa, maarifa na utaalamu miongoni mwa watumishi ili kuhakikisha Wizara inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Aidha, Maswi amewataka watumishi kuwa mstari wa mbele katika kubaini changamoto za wananchi na kutoa njia sahihi za kuzitatua.
“Maafisa Maendeleo ya Jamii ni wahamasishaji wa mabadiliko na kiungo muhimu kati ya Serikali na jamii, huku Maafisa Ustawi wa Jamii ni watoa huduma kwa jamii yetu hivyo ni wajibu wenu kutetea usawa na fursa kwa wananchi, kuratibu rasilimali zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali na kuwajengea wananchi uwezo wa kutekeleza majukumu yao, ikiwemo malezi na matunzo ya watoto na wazee”amesema Maswi.
Amesema watumishi wa Wizara hiyo ni jeshi la mageuzi ya kifikra kwa wananchi kwa sababu wanapowasaidia mwananchi kupata fursa, huduma na maarifa ya kukabiliana na changamoto, wanasaidia Serikali kutimiza wajibu wake.
Ameongeza kwamba watumishi wanapaswa kuhudumia wananchi kwa moyo wa huruma, uelewa wa dhana ya utumishi wa umma, uwajibikaji, nidhamu ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi na kuwaunganisha na huduma wanazohitaji kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya Maendeleo ya Jamii Ndayahundwa Balama amesema matarajio ya kikao kazi hicho ni kuimarisha Utendaji kazi miongoni mwa maafisa Maendeleo ya jamii na Wadau wa Maendeleo wanaotekeleza afua mbalimbali za Maendeleo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mtoto, Maadili na Malezi Asha Vuai amesema kikao kazi hicho kitasaidia watumishi hao kuwa na uelewa mpana katika kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Jamii ili kufikia malengo ya Dira2050.

