Nairobi, Kenya – Septemba 10, 2026 – Rais wa Kenya, William Ruto, amesisitiza dhamira ya Serikali yake ya kuhakikisha kunakuwa na mazingira ya biashara yanayotabirika, yenye uwazi na rafiki kwa wawekezaji, huku akieleza maendeleo katika mageuzi ya biashara na fursa mpya kwa wawekezaji wa Marekani katika sekta za viwanda, madini muhimu, teknolojia na biashara.

Rais Ruto amesema kauli mbiu ya Kenya kwa wawekezaji inajengwa katika utabirikaji wa mazingira ya biashara, kupitia mageuzi yanayolenga kupunguza vikwazo vya kikanuni, kuboresha utoaji wa leseni, kulinda uwekezaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika taasisi za Serikali. Amesema hayo wakati wa Mkutano wa Biashara wa AmCham 2026 ulioandaliwa na American Chamber of Commerce Kenya (AmCham Kenya) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi.

Amesema mkutano huo umefanyika katika kipindi ambacho mitaji ya kimataifa inatafuta maeneo mapya ya uwekezaji, huku Afrika ikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za ukuaji wa uchumi. Kwa mujibu wa Rais Ruto, Kenya inalenga kujenga mazingira ambayo wawekezaji wanaweza kutegemea kanuni zilizo wazi, leseni kutolewa kwa wakati, marejesho ya kodi kufanyika na mikataba kuheshimiwa.

Aidha, Rais Ruto amesema baadhi ya mageuzi yaliyotekelezwa tangu Mkutano wa mwaka 2023 ni pamoja na kuondolewa kwa VAT kwenye huduma zinazouzwa nje ya nchi, mabadiliko katika taratibu za marejesho ya kodi, mageuzi ya kodi kwa hisa za wafanyakazi pamoja na kuondolewa kwa sharti la umiliki wa ndani wa asilimia 30 kwa kampuni kubwa za teknolojia.

Amebainisha kuwa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje nchini Kenya umeongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.5 mwaka 2022 hadi dola bilioni 3.2 mwaka uliopita. Pia, karibu kampuni 100 katika maeneo maalumu ya kiuchumi (SEZ) zilizopewa leseni katika kipindi cha miaka minne iliyopita zimezalisha ajira 22,000 za viwandani.

Rais Ruto amesema mageuzi mengine yanayoendelea ni utekelezaji wa Sheria ya Taratibu Sawa za Utoaji Leseni za Kaunti, Muswada wa Uwekezaji na Uhamasishaji wa Mauzo ya Nje, mfumo wa kidijitali wa Kituo Kimoja cha Huduma za Uwekezaji pamoja na hatua za kurahisisha matakwa ya uzingatiaji wa sheria kwa wafanyabiashara.

Kwa upande wa uwekezaji kutoka Marekani, Rais Ruto amesema kampuni za Marekani zimewekeza zaidi ya dola milioni 600 katika miradi mipya tangu Mkutano uliopita wa mwaka 2024, akitaja kampuni za Oracle, Coca-Cola, Mars Wrigley na SC Johnson. Pia amesema kampuni ya Ford inaangalia fursa za uwekezaji nchini Kenya, hususan katika uzalishaji wa ndani na wa kikanda.

Amesema madini muhimu ni eneo jingine lenye fursa kubwa za uwekezaji, huku Kenya ikiwaalika wawekezaji kuwekeza siyo tu katika uchimbaji, bali pia katika uchakataji na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na madini kama rare earths, titanium, graphite na lithium.

Rais Ruto pia amekaribisha kuongezwa kwa muda wa mpango wa AGOA hadi Desemba 2028, akisema Kenya inalenga kujenga uhusiano wa kibiashara wa muda mrefu, wenye uwiano na manufaa kwa pande zote mbili kati yake na Marekani.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Frank W. Garcia Jr., amesema Afrika na Kenya kwa ujumla vipo katika hatua muhimu ya kimkakati inayoweza kuifanya Afrika kuwa miongoni mwa vinara wa uchumi duniani.

Garcia amesema sera ya Marekani kuhusu Afrika inabadilika kutoka mfumo uliolenga zaidi misaada kuelekea kwenye biashara, uwekezaji na ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote. Amesema Serikali ya Rais Donald Trump inalenga kujenga ushirikiano wa “win-win” na nchi za Afrika unaozingatia matokeo ya kibiashara na ustawi wa pamoja.

Kwa upande wake, Rais wa Bodi ya AmCham Kenya, Angela Ng’ang’a, amepongeza hatua zinazochukuliwa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha imani ya wawekezaji, akizitaka kampuni kutumia fursa za mageuzi hayo kupanua ushirikiano ndani ya Kenya na nje ya nchi.

Wakati wa mkutano huo, Kaimu Mkuu wa Ubalozi wa Marekani nchini Kenya, Susan Burns, alitangaza kusainiwa kwa makubaliano kadhaa, ikiwemo upanuzi wa shughuli za Digital Realty Afrika Mashariki kupitia ujenzi wa kituo cha data jijini Nairobi chenye thamani ya dola milioni 80 za Marekani.

Makubaliano mengine ni uzinduzi wa jukwaa la ufadhili wa usafiri linalotumia teknolojia ya blockchain, ushirikiano katika ukaguzi wa mizigo na usalama wa makontena, pamoja na kuimarishwa kwa ushirikiano katika sekta za ubunifu na usalama wa mtandao.

Aidha, Marekani imetangaza mradi mpya wa miaka mitano wenye thamani ya dola milioni 19.2 unaolenga kuboresha upatikanaji wa chakula bora na cha bei nafuu kwa mifugo nchini Kenya. Pia imetangazwa mashindano ya teknolojia kwa kampuni changa za Kenya, ambapo mshindi atapata fursa ya kwenda Marekani Mei 2027 kuwasilisha biashara yake kwa wawekezaji wakubwa wa mitaji na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wengine.

Mkutano wa Biashara wa AmCham 2026 ni wa siku mbili na unalenga kugeuza mijadala ya sera kuwa fursa halisi za kibiashara, ikiwemo kuongeza uwekezaji, kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda, kuunda ajira na kukuza biashara.