Mwamvua Mwinyi, Kibaha

Septemba 9, 2026

MEYA wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amekabidhi mashine ya photocopy kwa Shule ya Sekondari Mwambisi, hatua inayolenga kupunguza gharama kwa wazazi na wanafunzi wanaochangia fedha kwa ajili ya uchapishaji wa mitihani na nyaraka mbalimbali za kitaaluma.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyowakutanisha wazazi, walimu, wenyeviti wa bodi za shule, wanafunzi na wadau wa elimu, Dkt. Mawazo alisema ametoa mashine hiyo kutokana na changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo shuleni, akisisitiza umuhimu wa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya elimu.

Ameeleza utoaji wa mashine hiyo hauondoi wajibu wa wazazi na wadau katika kuchangia maendeleo ya shule, akieleza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Aidha, Nicas amemuagiza Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha kuchukua majina ya walimu wanaojitolea katika Shule ya Sekondari Mwambisi na kuangalia namna ya kuwasaidia kupata ajira za muda za kimkataba, akisema wameonesha uzalendo katika kutoa huduma ya elimu.

Nae Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha, Theresia Charles, alisema utoaji wa mashine hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za elimu, huku akitaja ukosefu wa mabweni katika shule nyingi za sekondari. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kibaha Mjini, Yahaya Mtonda, alimuomba Meya huyo kusaidia upatikanaji wa bweni na uanzishwaji wa kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari Mwambisi.

Mtonda aliwaasa wazazi kuimarisha malezi na kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kukabiliana na utoro na mmomonyoko wa maadili