Na Mwandishi wetu, Dar es Salaaam

WAKULIMA wakubwa, wa kati na wadogo nchini wanatarajiwa kupata fursa zaidi ya kutumia teknolojia ya ndege nyuki katika shughuli za kilimo, ikiwemo kunyunyiza viuatilifu na kufuatilia afya ya mazao.

Hatua hiyo inakuja baada ya kampuni ya Mati Technologies Company Ltd na Mazao Hub kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MOU), kwa lengo la kuwawezesha wakulima, hususan wakulima wadogo, kupata huduma za teknolojia hiyo inayozalishwa nchini.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa MOU hiyo, Mkurugenzi wa Mati Technologies, Benjamin Mollel, amesema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na majukwaa mbalimbali ya wakulima ili kupanua upatikanaji wa huduma za ndege nyuki na kuongeza tija katika kilimo.

Amesema Mazao Hub ni miongoni mwa majukwaa yanayowafikia wakulima wengi kupitia huduma zake za ugani na mfumo wa usambazaji wa pembejeo za kilimo, hivyo ushirikiano huo utasaidia kuunganisha wakulima na teknolojia kwa urahisi zaidi.

Mollel amesema lengo ni kuwafikia zaidi ya wakulima laki moja kote nchini ifikapo mwaka 2027, huku teknolojia hiyo ikilenga kusaidia wakulima kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake afisa mahusiano wa Mazao Hub Alexandra Ngaiza, amesema matumizi ya ndege nyuki katika kilimo yamekuwa yakihusishwa zaidi na wakulima wenye mashamba makubwa, lakini ushirikiano huo unalenga kubadilisha hali hiyo kwa kuwapa wakulima wadogo fursa ya kutumia teknolojia hiyo kupitia mifumo rahisi ya upatikanaji huduma ya Ndege nyuki hizo zinazozalishwa nchini.

Amesema teknolojia hiyo inaweza kusaidia kuongeza ufanisi katika unyunyiziaji wa viuatilifu, kuboresha uzalishaji na kupunguza uwezekano wa wakulima kukumbana moja kwa moja na kemikali wakati wa kunyunyizia mazao kwa njia za kawaida.

Mazao Hub, ambayo ni kampuni ya teknolojia ya kilimo (Agri-Tech), ambayo hutoa huduma za ugani kwa wakulima pamoja na kuwa na mfumo wa kuwaunganisha wakulima na pembejeo muhimu za kilimo, jambo linalowezesha teknolojia hiyo ya ndege nyuki zinazozalishwa nchini na Mati Technologies company ltd kuwafikia wakulima kupitia mtandao uliopo.