…………..

Watoto 16 wenye magonjwa ya moyo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu inayoendeshwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief Centre ya nchini Saudi Arabia.

Kambi hiyo maalumu imekusudia kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 30 wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, mishipa ya damu iliyopishana, pamoja na mishipa ya kupeleka damu kwenye mapafu kuziba kwa siku sita.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema ushirikiano kati ya JKCI na Taasisi ya King Salman kwa kipindi cha miaka 10 umekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watoto wenye magonjwa ya moyo walilofanyiwa upasuaji wa moyo nchini.

Dkt. Shonyela alisema wazazi na walezi wanapaswa kuwafikisha watoto hospitali mapema pale wanapowagundua kuwa na changamoto za kiafya ili kurahisisha matibabu yao na kupata huduma mapema.

Kwa upande wake daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya moyo kutoka Kituo King Salman Humanitarian Aid and Relief Centre ya nchini Saudi Arabia , Dkt. Aljohara Hamza, amesema timu hiyo ilianza kutoa huduma mara baada ya kuwasili JKCI na katika siku mbili za Jumamosi na Jumapili imefanikiwa kuwafanyia upasuaji watoto 11.

Dkt. Aljohara alisema kituo hicho kitaendelea kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana na madaktari wa JKCI kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa na watoto wengi wanapata huduma kupitia kambi hiyo.

“Tumefurahishwa na uwezo wa wataalamu wa JKCI katika kutoa huduma bingwa za upasuaji wa moyo kwa watoto, uwezo wao ni tofauti na tulivyoanza kushirikiana miaka 10 iliyopita”, alisema Dkt. Aljohara