KIONGOZI Mkuu wa Kanisa la Jesus Calling Mission International (JCMI) Arusha, Askofu Paulo Macha, ametoa wito kwa taasisi za kidini, mashirika, watu binafsi na wadau wengine kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani nchini, akisisitiza kuwa juhudi za pamoja zinaweza kuokoa maisha ya wagonjwa wengi.

Askofu Macha ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa True Rehoboth Cancer Foundation, uliofanyika katika Jengo la Ngome, Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo amesema jamii inapaswa kuwa na moyo wa kuwahudumia na kuwasaidia wagonjwa wa saratani, ikiwemo kuwapatia elimu, ushauri na msaada wa matibabu.

Amesema uzoefu wa maisha umemfundisha umuhimu wa kuwasaidia wengine, akieleza kuwa amewahi kumuombea mgonjwa aliyekuwa katika hali mbaya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye kuendelea kuishi na kupata nafasi ya kuendelea na huduma yake ya kuhubiri.

Askofu Macha pia amewapongeza madaktari na wahudumu wa afya kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwahudumia wagonjwa wa saratani, akisema wataalamu hao ni sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo na wanahitaji kuungwa mkono na jamii.

Amesema maandiko ya Biblia yanasisitiza umuhimu wa kuwahurumia wengine na kutoa, akitumia mifano mbalimbali ya kibiblia kueleza kuwa mtu mwenye uwezo wa kusaidia anapaswa kufanya hivyo kwa kuwa afya, mali na uwezo alionao ni sehemu ya baraka alizopewa na Mungu.

Kwa upande wake, Dkt. Kandali Samwel kutoka Idara ya Kinga na Elimu kwa Umma ya Taasisi ya Saratani Ocean Road (OCRC), amesema saratani ni changamoto kubwa nchini ambayo haiwezi kupuuzwa, hivyo juhudi za Serikali na wadau binafsi zinapaswa kuunganishwa ili kuongeza elimu, uchunguzi wa mapema na kuzuia ugonjwa huo.

Dkt. Kandali amesema changamoto kubwa inayowakabili wataalamu wa afya ni wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa katika hatua za tatu na nne za ugonjwa, hali inayoongeza gharama za matibabu na kupunguza uwezekano wa kupata matokeo mazuri ya matibabu.

Amesema tafiti zinaonesha kuwa kati ya asilimia 30 hadi 50 ya saratani zinahusishwa na matumizi na mifumo isiyofaa ya maisha, hivyo elimu kuhusu lishe bora, mazoezi na mtindo bora wa maisha inapaswa kupewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Dkt. Kandali ameipongeza True Rehoboth Cancer Foundation kwa kuanzisha mpango unaolenga kutoa elimu, kusaidia wagonjwa na kutoa ushauri nasaha, akisema huduma hizo zinaweza kupunguza mzigo wanaokutana nao wagonjwa na familia zao wakati wa matibabu.

Amesema OCRC iko tayari kushirikiana na taasisi hiyo pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha elimu ya saratani inawafikia wananchi wengi zaidi, huku akitoa wito kwa taasisi, kampuni, watu binafsi na wadau wote kuunga mkono mapambano hayo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa True Rehoboth Cancer Foundation, Lydia Mcharo, amesema taasisi hiyo imeanzishwa kutokana na uzoefu wake wa kukabiliana na saratani na kuona changamoto wanazopitia wagonjwa, hususan wale wanaokosa fedha, elimu, ushauri na msaada wa karibu kutoka kwa familia na jamii.

Mcharo amesema wakati wa matibabu yake katika Hospitali ya Ocean Road alikutana na wagonjwa waliokuwa katika hali ngumu, wengine wakiwa wamekata tamaa, wasio na ndugu wa kuwasaidia au wasiokuwa na uwezo wa kugharamia mahitaji mbalimbali, hali iliyomsukuma kuamua kuwasaidia wagonjwa wengine baada ya kupona.

Amesema kabla ya kuanzishwa rasmi kwa taasisi hiyo alikuwa ameshawasaidia zaidi ya wagonjwa 11 kwa njia mbalimbali, ikiwemo ushauri wa lishe, kuwatia moyo, kuwaombea na kuwafuatilia, hatua iliyomfanya kuona umuhimu wa kuanzisha chombo rasmi kitakachowaunganisha wadau wengi katika kuwasaidia wagonjwa wa saratani.

Mcharo amesema True Rehoboth Cancer Foundation, iliyosajiliwa mwaka 2025, inalenga kuziba pengo lililopo kati ya changamoto zinazowakabili wagonjwa na huduma wanazopata, ikiwemo ushauri nasaha, elimu ya kinga, lishe, mazoezi kwa wagonjwa na kuwawezesha wagonjwa kurejesha matumaini na hali ya kujiamini, huku akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya saratani yanahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali, wataalamu wa afya, taasisi na jamii.