NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke, amesema Uislamu si dini ya kuswali, kufunga na kwenda Hijja pekee, bali ni dini inayopaswa kutumika kutatua changamoto za watu na jamii, huku akitaka Maulid zitumike kudumisha amani na kuondoa mifarakano.
Alisema hayo jana jijini Mwanza, katika Maulid ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Ithna Asheriyyah Tanzania (TIC), akisisitiza kuwa waumini wanapaswa kuonyesha mafundisho ya dini kwa vitendo, hususan kuwasaidia wenye mahitaji.
Sheikh Kabeke alisema mtu anayekuja kuomba msaada wa matibabu anapopewa barua ya kuchangisha fedha, mchango huo unapaswa kumsaidia kutatua tatizo lake, akisema kutoa kiasi kidogo kisichokidhi mahitaji halisi ni kinyume na dhana ya kusaidiana katika dini.
“Tunaposhindwa kufanya kazi tusilete visingizio. Mnalalamika Shia wanachukua waumini wenu, ndiyo, wanafanya kazi. Haya mnayoyafanya ndugu zetu Washia yanatuamsha,” alisema.
Alisema Waislamu wanapaswa kuiga mfano wa Mtume Muhammad (S.A.W) katika kuwahudumia watu, akitaja historia ya Ahlus-Suffah, watu waliokuwa wakiishi karibu na Mtume na kupata msaada wa mahitaji yao, akisisitiza kuwa Uislamu unahimiza kuwajali wenye uhitaji.
Sheikh Kabeke alimpongeza Sheikh wa TIC Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hashimu Ramadhan, kwa msimamo wake wa kuhimiza amani na kufanya kazi, huku akimuomba Sheikh Mkuu wa TIC, Maulana Hemed Jalala, kufanya ziara Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuzungumza na Waislamu.
Akizungumzia suala la Katiba mpya, Sheikh Kabeke alisema Katiba iliyopo bado inatosha, huku akiwataka wananchi kuwa na subira na kusisitiza kuwa mabadiliko yanaweza kufanyika kwa ushirikiano na mazungumzo badala ya kuchochea migogoro.
“Katiba iliyopo inatosha. Tunaweza kufanya mabadiliko ya Katiba kwa kutoa ushirikiano badala ya kuwasha moto kwa wananchi. Hiyo si sawa,” alisema.
Aidha, Sheikh Kabeke alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za maendeleo, akisema baadhi ya watu wanamkosoa kwa sababu ya upole na huruma yake, huku akihoji kwa nini mambo mazuri anayoyafanya hayakutambuliwa kama baadhi ya watangulizi wake.
Alisema wanaotaka kuvunja sheria wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi, huku akiwataka Watanzania kuvumiliana licha ya tofauti zao, kwa kuwa migawanyiko hudhoofisha nguvu ya jamii na taifa.
“Dunia imebadilika. Yapo mambo yanayotuunganisha na yanayotutenganisha, hivyo tuvumiliane kwa yanayotutenganisha. Tunapogombana tunapoteza nguvu yetu kwa sababu ya kufarakana,” alisema.
Sheikh Kabeke pia alikumbusha kauli ya Rais wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi, aliyewahi kuwataka masheikh kuwa makini katika mijadala yao, akisisitiza umuhimu wa tofauti za kidini na kijamii kujadiliwa kwa hekima ili zisigeuke chanzo cha mifarakano.
Alisema Maulid yanapaswa kuwa fursa ya kujenga umoja, upendo na amani miongoni mwa Waislamu na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa mafundisho ya dini yanapaswa kuonekana katika matendo ya kuwasaidia watu na kutatua changamoto zao
