Hatimaye mji wa Mangaka unaenda kunufaika na mradi wa maji wa mji 28 uliofanikishwa na Serikali ambapo hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi itakuwa asilimia 100.
Mradi hu oni mahsusi katika kuongeza uzalishaji na kusambaza maji katika mji wa Mangaka na maeneo ya vijijini vya wilaya ya Nanyumbu yanayopitiwa na bomba kuu hivyo kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji.
Mradi una uwezo wa kuzalisha maji lita milioni tano (5,000,000) kwa siku na kuhudumia wakazi wapatao 81,000 walioko Nanyumbu mjini na vijiji vinavyopitiwa na bomba kuu. Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji inakuwa asilimia 100 katika mji wa Mangaka.
Thamani ya mradi wa miji 28 Mangaka ni takriban Dola za Marekani USD 16,380,000.59 na Serikali tayari imelipa Dola za Marekani USD 13,497,058.48.
Hivi sasa utekelezaji wa mradi umefika asilimia 96 na kwa kazi zifuatazo;
Ujenzi wa dakio (intake) umefika asilimia 96, Ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji (WTP) upo asilimia asilimia 94, ulazaji wa bomba kubwa kutoka katika mtambo wa kuchuja maji (WTP) mpaka katika tanki la Sengenya umekamilika kwa asilimia 100, ulazaji wa mtandao wa kusambaza kwa maji kwa wateja upo asilimia 96 na ujenzi wa tenki (100m3) la kusambaza maji kijiji cha masuguru 94%
Majaribio ya kwanza na ya pili yameshafanyika ya kutoa maji kutoka kwenye dakio hadi tanki la kusambaza maji la Sengenya lenye ujazo wa lita milioni moja.. Hatua inayoendelea ni majaribio ya teknolojia ya scada pamoja na majaribio ya kusukuma maji yaliyotibiwa kutoka eneo la chujio (treatment plant) hadi kwenye mabomba ya usambazaji mjini Mangaka. Pia, majaribio mbalimbali ikiwemo majaribio ya line kubwa ya kutoa maji Masuguru kuelekea tanki la Sengenya.
Mradi wa Miji 28 unatekelezwa na Wizara ya Maji kupitia mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA). Ni mradi mkubwa wa kutoa maji katika mto Ruvuma kuhudumia wakazi wa mji wa Mangaka pamoja na vijiji vyote vya pembezoni mwa mji na vijiji vinavyopitiwa na bomba kuu. Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya M/S AFCON Infrastructure na mkandarasi mshauri WAPCOS LTD kutoka nchini India.

