Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Malengo Development ,Hamza Rajabu akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo.

………… 

Happy Lazaro,Arusha 

Arusha.ZAIDI ya vijana 500 wamenufaika na elimu ya ujuzi na ujasiriamali kuanzia mwaka 2022 hadi 2026 na kuweza kujikwamua kiuchumi kwa kuweza kujiajiri wenyewe.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Malengo Development ,Hamza Rajabu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .

Amesema kuwa,shirika hilo limekuwa likiwezesha vijana katika kujikwamua kwenye changamoto mbalimbali za umaskini kwa kuwapatia elimu ,ujuzi,na kuwawezesha kupata huduma bora za kiafya.

“Tumekuwa tukifanya kazi katika wilaya za Arusha,Meru,Arusha dc,Monduli na Karatu ambapo vijana hao wameweza kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ambayo imewawesha kujipatia kipato.”amesema Hamza.

Amesema kuwa,wamekuwa wakitoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 35 chini ya chuo cha MADIVOTEC Institute ambapo kwa mwaka wamekuwa wakifikia vijana 150.

“Tumekuwa tukifundisha vijana maswala mbalimbali ikiwemo maswala ya kuchomolea ,kompyuta,ambapo wakimaliza tumekuwa tukiwafundisha namna ya kujiunga kwenye vikundi na kuwaunganisha na halmashauri ili kupata mikopo “amesema Hamza.

Amesema kuwa,mbali.na huduma hizo wanazotoa wamekuwa wakitoa huduma ya elimu ya awali bure kwa watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu kuanzia miaka 2 hadi 5 kupitia taasisi ya The Make Academy ambapo tangu waanze huduma hiyo mwaka 2025 wameshahudumia watoto 200 hadi sasa hivi.

“Mbali na kusaidia watoto hao pia tumeweza kusaidia wazazi wao kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali na namna ya kulea watoto ambapo kwa mwaka tumekuwa tukihudumia wamama 40 ambapo tumeweza pia kuwafundisha kilimo cha mbogamboga,kushona nguo pamoja na kutengeneza vitafunio na lengo kubwa ni ili waweze kujihudumia wenyewe na kuondokana na changamoto mbalimbali za kipato. “amesema Hamza.

Ameongeza kuwa,wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa wazazi wa watoto hao kwa kipindi cha miezi sita na kuwafundisha namna ya kujiunga na vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya halmashauri.