Dar es Salaam

Wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Kisarawe Seminari (Kisarawe Lutheran Junior Seminary) wametembelea ofisi za HESLB hivi karibuni, ambapo wamepata elimu na uelewa wa kina kuhusu mchakato wa uombaji mikopo ya elimu ya juu pamoja na urejeshaji wa mikopo iliyoiva.

Wanafunzi hao, walipokelewa na kupata fursa ya kujifunza kwa hatua mbalimbali kuhusu namna HESLB inavyotekeleza majukumu yake katika kuwezesha wanafunzi wenye sifa kupata mikopo ya elimu ya juu.

Katika ziara hiyo, wanafunzi hao walielekezwa kuhusu mchakato wa maombi ya mikopo, kuanzia dirisha la maombi linapofunguliwa, namna ya kuwasilisha maombi na taarifa muhimu, uchakataji na uhakiki wa maombi, hadi hatua ya kupangiwa na kutolewa kwa fedha za mkopo kwa wanafunzi wenye sifa.

Aidha, walipata elimu kuhusu upande wa urejeshaji wa mikopo iliyoiva ambapo walielezwa namna wajibu wa kurejesha mkopo unavyoanza baada ya mwanafunzi kukamilisha masomo ya elimu ya juu, pamoja na umuhimu wa kutambua kuwa mkopo ni uwezeshaji unaopaswa kurejeshwa ili kuwawezesha wanafunzi wengine.

Kwa upande wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Brian Charles Urio, amesema ziara hiyo imewasaidia kuondokana na dhana na taarifa ambazo si sahihi kuhusu vigezo vya mikopo ya elimu ya juu.

“Tumefurahi sana kupata nafasi hii ya kutembelea HESLB. Tulichokiona katika utendaji kazi na elimu tuliyopata hapa ni tofauti na baadhi ya taarifa tunazozisikia mtaani. Tumepewa elimu ya moja kwa moja na tumeelimishwa namna mchakato wa mikopo unavyofanyika, maarifa haya yatatusaidia kufanya maamuzi sahihi tunapofikia hatua ya kuomba mikopo na pia kuwaelimisha wenzetu,” amesema Urio.

Wanafunzi hao pia wameahidi kuwa mabalozi wazuri wa HESLB kwa kuwafikishia wenzao na jamii kwa ujumla taarifa sahihi kuhusu mikopo ya elimu ya juu, hususan katika kipindi ambacho taarifa potofu kuhusu mikopo zinaweza kuwafanya baadhi ya wanafunzi kukata tamaa au kufanya maamuzi yasiyo sahihi.

Ziara hiyo imekuwa sehemu muhimu ya kuwajengea wanafunzi uelewa mapema kuhusu fursa za elimu ya juu, taratibu za mikopo na wajibu wa mnufaika, na umuhimu wa kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo rasmi.

Wanafunzi hao wametanabaisha kwamba, ziara yao HESLB haikuwa tu matembezi ya kielimu, bali ilikuwa darasa la vitendo lililowapa mwanga kuhusu safari yao ya elimu ya juu na namna wanavyoweza kunufaika na huduma za mikopo kwa uelewa sahihi na uwajibikaji.

Wanafunzi hao wa kidato cha sita ni kutoka tahasusi za PCB, PCM, EGM na HGL.