Dar es Salaam, Septemba 3, 2026
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa taasisi, kampuni, mashirika na wadau wa maendeleo kujitokeza kudhamini Samia Kalamu Awards 2026 ili kuunga mkono uandishi wa habari unaochochea maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 3, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda, wakati akitangaza kufuzu kwa kazi 294 zilizoingia katika hatua ya kupigiwa kura na wananchi.
Mhandisi Mwasalyanda amesema ushiriki wa wadau kupitia udhamini ni sehemu muhimu ya juhudi za kutambua, kuenzi na kuhamasisha uandishi wa habari wenye ubora, weledi na ubunifu pamoja na maudhui yenye manufaa kwa jamii.
Amesema udhamini wa tuzo hizo utasaidia kujenga na kuimarisha mazingira yatakayowahamasisha waandishi wa habari na vyombo vya habari kuendelea kuzalisha maudhui bora, yenye taarifa sahihi na yanayozingatia maadili ya taaluma.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuunga mkono Samia Kalamu Awards ni kushiriki katika juhudi za kukuza uandishi wa habari unaochangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitaifa.
Katika msimu wa mwaka 2026, kazi 3,003 kutoka kwa waombaji 985 ziliwasilishwa kwa ajili ya kushindanishwa. Baada ya tathmini ya jopo la majaji, kazi 294 zilizopata alama za juu zimefuzu kuingia katika hatua ya kupigiwa kura na wananchi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt, Rose Reuben amewakaribisha wananchi kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa kuwa wananchi ndio walaji wa habari na kutambua maudhuri ambayo yamewaguswa katika maeneo yao na kuamua kama zinaweza kushinda.
“Kura ya wananchi ni ya muhimu sana kwa sasa kwa kuendeleza na kutambua maudhui ya ndani, kwa kuitangaza nchi kutambulika kimataifa kupitia habari zilizondikwa kwa weledi na waandishi wa habari mahiri walioshiriki katika shindano la SKA 2026″. Dkt Rose Reuben – Mkurugenzi Mtendaji TAMWA
“Kwa tathmini yetu ya majaji wa SKA 2026 wakati tunapitia makala zilizowasilishwa tumebaini kuwa waandishi wa habari wa Tanzania wanauwezo mkubwa wa kuibua masuala mbalimbali ya maendeleo katika ngazi zote nchini”. Mmoja wa majaji SKA 2026 Bi, Beatrice Bandawe
Tuzo za Samia Kalamu Awards zinajumuisha makundi mbalimbali yanayowapa waandishi wa habari, maafisa habari na vyombo vya habari fursa ya kushindana kupitia kazi zilizochapishwa au kurushwa ndani ya kipindi kilichobainishwa.
Tuzo hizo zinaratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na TAMWA na JAB, chini ya kaulimbiu ya “Kalamu kwa Maendeleo.”

