MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Jaffer Machano, amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika vipande vya Makutupora–Tabora, Tabora–Isaka na Isaka–Mwanza, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati.

Bw. Machano ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika vipande vya tatu, vinavyohusisha Makutupora hadi Tabora, kipande cha nne kutoka Tabora hadi Isaka na kipande cha tano kutoka Isaka hadi Mwanza.

Amesema ziara hiyo imewapa fursa wajumbe wa Bodi kujionea kwa vitendo maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kupata taarifa kutoka kwa menejimenti ya TRC pamoja na wakandarasi wanaotekeleza kazi.

“Tumetembelea kuanzia kipande cha tatu mpaka cha tano na tumefurahishwa na maendeleo ya ujenzi. Tunategemea kwamba kasi ya maendeleo ya mwezi hadi mwezi itaendelea kuwa nzuri na kuwa na mwelekeo unaokubalika,” amesema Bw. Machano.

Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto ndogo zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi, Bodi imewataka wakandarasi kuongeza kasi ya kazi, ikiwemo kuongeza zamu za usiku, ili kuhakikisha muda uliopangwa wa kukamilisha mradi unazingatiwa.

“Tunawaelekeza kuongeza kasi na kuongeza zamu za usiku. Tumeongea nao na tumekubaliana kwamba wataweza kutimiza kazi kwa muda ambao tumepanga,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Masanja Shiwa, amesema ujenzi wa SGR katika vipande hivyo unaendelea na kwamba hakuna sehemu ambayo ujenzi umesimama.

Amesema changamoto kubwa iliyopo katika baadhi ya maeneo ni pamoja na kuingia katika miji mikuu ambako kuna mwingiliano wa shughuli za kijamii na miundombinu iliyopo, hali inayohitaji wananchi walio katika maeneo ya mradi kuondolewa na kulipwa fidia ili kuruhusu ujenzi kuendelea.

Mhandisi Shiwa amesema katika kipande cha tano cha Isaka–Mwanza, mradi umeendelea kwa kasi, huku kazi mbalimbali za ujenzi zikiendelea katika maeneo tofauti kuelekea Mwanza.

Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza kwa maandalizi mwaka 2020 na baadaye kasi ya ujenzi kuongezeka, huku changamoto mbalimbali za kiuchumi na upatikanaji wa vifaa duniani zikiwa miongoni mwa mambo yaliyowahi kuathiri utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Amesema TRC inaendelea kushirikiana na wakandarasi na wahandisi kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi na kazi zinaendelea kwa kasi inayohitajika.

“Tunataka kuhakikisha jambo hili linaendelea vizuri. Hata changamoto za hali ya hewa tutazizingatia katika kupanga programu ya ujenzi ili zisitukwamisha na kuhakikisha kazi inaendelea,” amesema Mhandisi Shiwa.

Katika ziara hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TRC imepata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali ya mradi, ikiwemo miundombinu ya reli, madaraja na vituo, hatua ambayo imeelezwa kuwa inalenga kuijengea Bodi uelewa wa kina kuhusu utekelezaji wa mradi na changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

Mradi wa SGR kutoka Makutupora hadi Mwanza ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kujenga mtandao wa reli ya kisasa unaolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo, kupunguza gharama za usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya TRC, utekelezaji wa kipande cha Mwanza–Isaka ulikuwa umefikia asilimia 68 Februari 2026, huku lengo likiwa ni treni ya kisasa kuanza kusafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza ifikapo mwaka 2028.