Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la  Smarticents , Klein  August akizungumza kwenye jukwaa hilo jijini Arusha
……………
Na Happy Lazaro, Arusha 
Vijana  nchini  wametakiwa kutumia majukwaa ya mafunzo, semina na mijadala mbalimbali kama fursa ya kujifunza, kujenga mitandao na kutafuta njia mpya za kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamesemwa jijiji Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la  Smarticents , Klein  August
 wakati akizungumza katika Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Arusha, lililowakutanisha viongozi wa Serikali, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo kujadili nafasi ya NGOs katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Klein amesema shirika hilo  limejikita katika kutoa elimu ya fedha kwa vijana pamoja na makundi maalumu  katika jamii, huku ikiendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kusimamia shughuli zao na kuongeza kipato.
Amesema kuwa, ushiriki wake katika tukio hilo umempa nafasi ya kujifunza namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya mashirika, taasisi na serikali ili kutumia vizuri rasilimali zilizopo na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa,moja ya maeneo muhimu waliyojifunza ni matumizi ya teknolojia na akili bandia (AI) katika kuboresha namna ya kutumia na kuhamasisha rasilimali huku  akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ili waweze kutumia fursa zinazojitokeza katika uchumi wa sasa.
Kwa upande wa fursa zinazotarajiwa kujitokeza kuelekea michuano ya AFCON, Klein amesema shirika hilobado linaendelea kuchakata namna bora ya kuwawezesha vijana kuzitambua na kuzitumia fursa hizo, na kusisituza maandalizi yanapaswa kuanza kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi unaohitajika.
Amefafanua  kuwa, kupitia semina na mafunzo ya vitendo, vijana wataweza kujifunza namna ya kutambua fursa, kujenga mahusiano ya kibiashara na hata kujua namna sahihi ya kumkaribia mgeni au mwekezaji anayekuja nchini ili kubadilisha uwepo wake kuwa fursa ya biashara na kipato.
“Yawezekana kijana anataka kujua namna ya kuzungumza na  mtu ambaye ni mgeni amekuja nchini, na kujua namna ya kufanya naye biashara ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kumpatia kipato,” amesema.Klein .
Aidha Klein ameishukuru Serikali na wadau mbalimbali walioandaa jukwaa hilo na kusema kuwa, majukwaa kama hayo ni muhimu kwa vijana kwa sababu yanawawezesha kupata maarifa, kukutana na watu wenye uzoefu na kupata ushauri unaoweza kuwasaidia kupanga na kujenga maisha yao ya baadaye.