Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma

Serikali imewataka wananchi hususan vijana, kupunguza matumizi ya pombe yaliyokithiri na kuacha matumizi ya dawa za kulevya ili kuepuka changamoto za afya ya akili pamoja na madhara mengine kwa familia na jamii. 

Wito huo umetolewa leo Septemba 02, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati akifungua mafunzo kwa wataalaamu wa afya ya akili yaliyofanyika Mkoani Dodoma yenye lengo la kuongeza huduma za kinga na matibabu kwa waraibu.

“Matumizi ya pombe yaliyokithiri ni miongoni mwa changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele, hasa kutokana na vijana kuanza kutumia pombe katika umri mdogo ambapo hali hiyo inaweza kuathiri masomo, kazi, mahusiano ya kifamilia na uwezo wa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za jamii,” amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema matumizi yaliyokithiri ya pombe na dawa za kulevya yanachangia vitendo vya ukatili na migogoro katika jamii, huku akisisitiza kuwa mtu anapofikia hatua ya utegemezi mkubwa wa vilevi, kumsaidia kuacha si jambo rahisi na kunahitaji wataalamu, matibabu, muda pamoja na ushirikiano wa familia na jamii na jamii inayomzunguka. 

Amesema, serikali imeendelea kuongeza vituo vinavyotibu uraibu kutoka kituo 1 hadi vituo 14 na huduma hizo kwa sasa zinaendelea kusogezwa ngazi za chini walipo wananchi ambapo amesisitiza kuwa huduma hizi zitolewe bila unyanyapaa wala ubaguzi na kushirikiana na wamiliki wa vituo vya utengemao (Sober houses) ili kuwafikia waathirika wengi zaidi. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamadi Nyembea amesema mafunzo hayo yatasaidia jamii kwakuwa yanakwenda kutolewa kwa wataalamu wa afya katika mikoa 17, hususan katika maeneo yenye matumizi makubwa ya pombe. 

Mwisho, Dkt. Nyembea amesema jukumu la wataalamu wa afya ni kuwatambua wenye changamoto mapema, kutoa huduma za awali na kuwapeleka katika vituo vya ngazi za juu pale wanapohitaji huduma za kibingwa zaidi, hatua itakayosaidia wananchi kupata huduma kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi.

Serikali imesisitiza kuwa watu wenye changamoto za afya ya akili hawapaswi kunyanyapaliwa wala kutengwa, bali wanapaswa kusikilizwa, kusaidiwa na kupewa nafasi ya kurejea katika maisha ya kawaida, matibabu ya afya ya akili si dawa pekee, bali yanapaswa kuhusisha familia, jamii na mazingira ambayo mgonjwa anaishi.