NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Fabian Ngajilo, ameiomba Serikali kuharakisha uhamishaji wa Gereza Kuu la Iringa kutoka eneo la mjini kwenda Mlolo, Kata ya Isakalilo, ili kupisha upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Ngajilo ametoa ombi hilo Bungeni wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayub Mohamed Mahamud, baada ya Serikali kueleza kuwa mchakato wa kuhamisha gereza hilo unaendelea
.
Ngajilo amesema suala la kuhamisha Gereza Kuu la Iringa limejadiliwa kwa muda mrefu, akieleza kuwa mjadala huo umeanza tangu miaka ya 1980, huku eneo la Mlolo likiwa tayari limetengwa kwa ajili ya ujenzi na uhamisho wa gereza hilo.
Amesema uwepo wa gereza katika eneo la mjini umeendelea kuwa kikwazo katika upanuzi wa huduma za Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, licha ya eneo hilo kuwa muhimu kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya.
Ngajilo amesema yeye kwa kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa wamefanikiwa kupata Sh milioni 600 kutoka shirika la maendeleo la Italia kwa ajili ya kujenga jengo kubwa la huduma ya tiba ya viungo (physiotherapy), lakini utekelezaji wa mradi huo umekwama kutokana na kukosekana kwa eneo la kujenga.
“Tumeshapata milioni 600 kutoka shirika la maendeleo la Italia kwa ajili ya kujenga jengo kubwa la physiotherapy. Sasa hatuna eneo la kujenga kwa sababu magereza bado wako pale pale,” amesema Ngajilo.
Amesema taasisi nyingine zilizokuwa katika eneo hilo tayari zimeondoka, huku Gereza Kuu la Iringa likiwa miongoni mwa taasisi zilizobaki katika eneo linalohitajika kwa ajili ya upanuzi wa hospitali.
Kutokana na hali hiyo, Ngajilo amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuweka tarehe maalum ambayo Serikali itahakikisha Gereza Kuu la Iringa linaondoka mjini na kuhamia Mlolo.
“Niombe Mheshimiwa Waziri uweke sasa tarehe ya lini wataondoka magereza pale Iringa mjini,” amesema.
Mbali na suala la uhamishaji wa gereza, Ngajilo pia ameiomba Serikali kupitia Jeshi la Magereza kuharakisha mchakato wa kuhamisha mipaka katika eneo la Mlolo, ambako amesema kulikuwa na mgogoro wa nyumba 75 zilizokuwa ndani ya eneo la magereza.
Amesema mgogoro huo tayari umeshatatuliwa na kinachosubiriwa sasa ni hatua za mwisho za kurekebisha mipaka ili wananchi hao waweze kupata hati za maeneo yao na kumiliki ardhi kwa uhalali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahamud, amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuhamisha gereza hilo na inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha mpango huo unatekelezwa.
Amesema Serikali kupitia Jeshi la Magereza tayari imeanza kujenga miundombinu katika eneo la Mlolo kwa ajili ya kuwezesha uhamisho wa Gereza Kuu la Iringa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ilitenga Sh milioni 183 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, na kufanya jumla ya mabweni katika eneo hilo kufikia manne.
Amesema mabweni hayo yamejengwa na kwa sasa yako katika hatua za mwisho za ukamilishaji, huku nyumba 20 za maafisa na askari wa magereza zikiwa zimejengwa na kukamilika.
Naibu Waziri amesema uamuzi wa kuhamisha gereza hilo unatokana pia na umuhimu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na changamoto za kiusalama zinazoweza kujitokeza kutokana na ukaribu wa gereza na hospitali.
Amesema uwepo wa gereza karibu na hospitali umekuwa ukisababisha wakati mwingine barabara kufungwa kwa sababu za kiusalama, hali ambayo huathiri matumizi ya barabara kwa wananchi pamoja na shughuli za hospitali.
Naihu Waziri Mahamood amesema Serikali bado haijaweka tarehe maalum ya uhamishaji wa gereza hilo kwa sababu inaendelea na juhudi za kutafuta fedha za kukamilisha miundombinu inayohitajika katika eneo la Mlolo.
Amesema Serikali inatambua uhitaji mkubwa wa magereza nchini na kwamba suala la bajeti ni moja ya mambo yanayoathiri kasi ya utekelezaji wa mpango huo.
Naibu Waziri amempongeza Ngajilo kwa kuendelea kufuatilia suala hilo na kutetea upanuzi wa huduma za afya kwa wananchi wa Iringa, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua zinazohitajika ili kukamilisha mpango wa uhamishaji wa Gereza Kuu la Iringa.
