CHUO kikuu kinatarajiwa kujengwa kwenye Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wanaoishi kwa wingi jamii ya wafugaji na wakulima.
Mratibu wa shirika lisilo la kiserika la Ujamaa Community Resource Team (UCRT) Edward Loure ameeleza hayo kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Noomunyi Kijiji cha Loiborsiret.
Loure ameeleza kuwa wanatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika suala la elimu ili kuwarithisha watu wa jamii ya eneo hilo na watanzania kwa ujumla.
Amesema wanatarajia kujenga chuo kikuu kwemye eneo la Ndepes katika kata ya Loiborsiret, ambapo watasoma wakazi wa eneo hilo na watanzania kwa ujumla.
“Tukijenga chuo kikuu hapa Loiborsiret ambapo itakuwa karibu na makazi ya eneo hilo na faida kubwa na manufaa kwa jamii kwani wasomi wetu wataongezeka eneo hili,” amesema Loure.
Amesema elimu ni jambo la msingi kwani japokuwa wazazi wake hawakupata elimu akiwemo baba yake na mama zake saba ila yeye alibahatika kusomeshwa na Kanisa Katoliki.
“Baba yangu alichangia elimu yangu kwa kutoa ndama jike mmoja na sasa hivi ndugu zangu 30 au 40 mimi natumia shilingi milioni 70 kuwachangia kwa mwaka ili wasome,” amesema Loure.
Amesema chuo kikuu kitakachojengwa Loiborsiret kitakuwa ni maono makubwa kwao hivyo jamii ya eneo hilo waunge mkono hilo.
