Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

CHUO Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kimeendelea kuimarisha na kupanua Shamba la Mafunzo la Chuo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi, wakulima na wadau wengine kupata maarifa na ujuzi wa kilimo kupitia mafunzo ya vitendo.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 31, 2026 Jijini Dodoma, wakati akieleza utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael T. Chibunda, amesema shamba hilo limeandaliwa kuwa eneo muhimu la mafunzo, utafiti na uendelezaji wa teknolojia mbalimbali za kilimo.

Amesema shamba hilo lina vitengo mbalimbali vinavyohusisha uzalishaji wa mazao, mifugo, utafiti na mafunzo ya uchumi wa buluu pamoja na kilimo cha matunda na mboga.

Prof. Chibunda amesema SUA pia imeweka kitengo maalumu cha hifadhi ya mazao yanayopatikana katika kanda mbalimbali za Tanzania, yakiwemo mazao ya kimkakati kama miwa, korosho, chikichi, zabibu, kahawa, pamba, chai, katani, kakao na nazi, pamoja na miti mbalimbali ya matunda.

Amesema eneo hilo pia lina mifugo mbalimbali inayotumika katika mafunzo na utafiti, ikiwemo samaki aina ya sato na kambale, ng’ombe, mbuzi, kuku, kondoo, ngamia, farasi na sungura.

Aidha, amesema SUA imeendelea kuimarisha mafunzo ya kilimo biashara na ujasiriamali kupitia Kituo cha Atamizi, ambacho kinatumia vitalu nyumba 91 na vitalu 20 vya kilimo cha nje kuwajengea vijana uwezo wa kuzalisha kibiashara.

Katika kuendana na mahitaji ya sekta ya kilimo na soko la ajira, Prof. Chibunda amesema kupitia Mradi wa HEET, SUA imefanya mapitio na kuboresha mitaala 111, ambayo tayari imepata ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), huku mitaala sita ikiwa ya mafunzo ya amali.

Aidha, amebainisha Kuwa SUA inaendelea kuandaa mitaala mingine 11 kwa ajili ya kuongeza idadi ya wanafunzi katika Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi, hatua inayolenga kupanua fursa za elimu ya juu na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya sekta ya kilimo na maendeleo ya Taifa.

Amebainisha Kuwa hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa SUA kuhakikisha elimu ya kilimo haiishii darasani pekee, bali wanafunzi na wadau wanapata ujuzi wa vitendo unaoweza kuongeza uzalishaji, kukuza kilimo biashara, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.