Muleba, Kagera

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2026 Wazo Michael Mwang’onda amepongeza ubunifu wa wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ubunifu na kuhakikisha wananchi wa wilaya ya Muleba wanaendelea kunufaika na miundombinu ya barabara 

Pongezi hizo amezitoa wakati akizindua barabara ya Marahala – MSD yenye urefu wa Km. 0.49 kwa kiwango cha lami ambayo itarahisisha mawasiliano kati ya wananchi wa vijiji wa Magata Nshamba, Muleba mjini na Hospitali ya Wilaya ya Muleba.

Amesema serikali itaendelea kutekeleza miradi ya barabara kwa wanachi wavijiji ili kurahisisha mawasiliano biashara na uchumi huku akiwataka wananchi kutumia fursa zilizoko katika miradi ya barabara inayotelezwa kuinua uchumi wao.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilaya ya Muleba Dativa Semforini amesema kwa sasa barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 100 na kuwekewa taa za barabarani na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kibiashara muda wote.

Amesema pia barabara hiyo imerahisisha huduma za Bohari ya Dawa (MSD) ambapo hapo awali barabara hiyo ilikuwa na changamoto kutokana na magari makubwa kufanya shughuli zake katika bohari hiyo.

Baadhi ya wananchi wanaotumia barabara hiyo kwa sasa akiwemo Seif Mzamiri amesema kuwa serikali imetatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa barabara kwa kiwango cha lami.

Amesema mara baada ya kuweka lami katika barabara hiyo wameshuhudia ujenzi wa hospital ukienda kwa kasi na sasa hospital imekamilika hivyo wanaamini 

uwepo wa barabara hiyo itarahisha shughuli za afya masoko na mahitaji yote ya kijamii na kiuchumi.