Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

KAIMU Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi, Bw. Gwakisa Bapala, amesema zaidi ya Watanzania milioni 11 wamefikiwa na huduma mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi, wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.Ameyasema hayo Agosti 31, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano la Tano la Ushiriki wa Watanzania kwenye Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji, litakalofanyika Septemba 2 na 3, 2026 Jijini Dodoma.

Amebainisha kuwa kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi kujadili fursa za kisera, kimiradi, ajira, bidhaa, huduma na uwekezaji zinazopatikana katika miradi ya kimkakati.

Ameongeza kuwa kongamano hilo litakuwa na zaidi ya washiriki 500 na halitakuwa na kiingilio, huku mgeni rasmi anararajiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.

Aidha ,amesema kongamano hilo litashirikisha taasisi mbalimbali ikiwemo PURA, Tume ya Madini na TPDC, huku Benki ya CRDB ikiwa mdhamini mkuu.

Pia amebainisha kuwa makongamano yaliyopita yamechangia kuongeza ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati, akitoa mfano wa Mradi wa Julius Nyerere ambapo zaidi ya asilimia 95 ya ajira zimetolewa kwa Watanzania, pamoja na kampuni za Kitanzania kushiriki katika kazi za subcontracting.

Huku akibainisha Kuwa kupitia jitihada hizo, sera, sheria na kanuni zimeboreshwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo madini, mafuta na gesi, huku Serikali ikiwa katika hatua za mwisho za kutunga National Local Content Policy.

Aidha, amesema katika kongamano hilo utazinduliwa mfumo wa National Empowerment Management Information System, utakaotoa taarifa za fursa za ajira na ushiriki katika miradi ya kimkakati, uwekezaji wa ndani na uwekezaji kutoka nje, pamoja na kutolewa tuzo kutambua jitihada za Serikali katika kuwawezesha Watanzania kushiriki kwenye miradi hiyo.