NA DENIS MLOWE, IRINGA
DIWANI wa Viti Maalum Kanda ya Kihesa, Sarah John Ponela, amewataka wazazi na walimu kushirikiana kwa karibu katika malezi na elimu ya watoto ili kujenga kizazi chenye nidhamu, heshima na uwezo wa kulitumikia taifa.
Ponela alitoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya Shule ya Awali ya Fransis iliyopo mjini Iringa, akisema malezi ya watoto hayawezi kuachiwa upande mmoja pekee, bali yanahitaji ushirikiano kati ya wazazi, walimu, wadau na Serikali.
Alisema uzoefu wake kama mzazi umemfanya kutambua ukubwa wa kazi inayofanywa na walimu, ambao hukaa na watoto kwa muda mrefu na kuwafundisha taaluma pamoja na maadili.
“Taifa hili ni la kwetu, watoto hawa ni wa kwetu. hatuna watoto wengine, Mungu ametupa zawadi hii tushirikiane vizuri na walimu mashuleni ili kuleta taifa ambalo tunalitegemea,” alisema Ponela.
Ponela, ambaye pia ni mhandisi wa ujenzi na mjumbe wa kamati za elimu, afya na uchumi katika Manispaa ya Iringa, alisema yuko tayari kusaidia kufikisha changamoto zinazolikabili shule hiyo katika ngazi za Serikali na kushirikiana na wazazi na wadau kuzitatua.
Aidha, aliitaka shule hiyo kuweka mpango wa kuanzisha shule ya msingi ili watoto wanaomaliza elimu ya awali waweze kuendelea na masomo katika mazingira yale yale na kudumisha misingi ya elimu na maadili wanayofundishwa.
“Hebu tukaa na kamati yako, tuite wadau kama ulivyosema, tujaribu kuweka hilo kwa ajili kuanzisha primary. tuanze nao awali mpaka msingi,” alisema.
Akizungumzia changamoto za shule hiyo, Ponela alitaja upungufu wa vifaa vya michezo, meza na viti, jiko, vyumba vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu, akisisitiza kuwa wazazi ndio wadau wa kwanza katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Alieleza kuwa mchango wa maendeleo si lazima uwe fedha pekee, bali unaweza kuwa vifaa, nguvu kazi au rasilimali nyingine zinazohitajika katika ujenzi na uboreshaji wa mazingira ya shule.
Katika kuunga mkono jitihada hizo, Ponela alikabidhi carpet yenye thamani ya karibu Sh500,000 kwa ajili ya matumizi ya watoto shuleni, baada ya kusikia ombi la shule kuhusu uhitaji wa vifaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule ya Awali ya Fransis, Mchungaji John Mwaigwisya, alimpongeza Ponela kwa kile alichokiita kuwa ni kiongozi wa vitendo, akisema mchango huo umeonyesha kuwa shule hiyo ina wadau wanaounga mkono maendeleo yake.
Mwaigwisya pia aliunga mkono wazo la kuanzisha shule ya msingi, akisema hatua hiyo itawasaidia watoto wanaomaliza elimu ya awali katika shule hiyo kuendelea na masomo bila usumbufu na kuhakikisha wanaandaliwa kwa misingi iliyowekwa na shule.
Alisema shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2009 ilikuwa na wanafunzi 22, lakini hadi mwaka 2026 imefikia takribani wanafunzi 450, hatua aliyosema inaonyesha ukuaji wa shule na imani ya wazazi katika huduma inayotolewa.
Katika risala yao, wanafunzi waliwataka wazazi, walezi na wadau kuendelea kuiunga mkono shule hiyo, hasa katika upatikanaji wa vifaa vya michezo vinavyokadiriwa kugharimu Sh450,000.
Walisema pamoja na mafanikio katika elimu, nidhamu na ukuzaji wa vipaji kupitia michezo, kuimba na kuchora, bado shule inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya michezo.
Wanafunzi hao pia waliwaahidi wazazi na walimu kuendelea kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kuwaheshimu wazazi na walimu wao ili kutimiza ndoto zao na kuwa watu wenye manufaa kwa familia na taifa.

