Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog,Dodoma
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazohusu miundombinu ya umeme, ikiwemo matukio ya uharibifu na hujuma dhidi ya miundombinu hiyo.
Akizungumza Agosti 27, 2026, baada ya watumishi wa Idara ya Mahakama, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Wasajili, Mahakimu, Watendaji na wafanyakazi wengine kufanya ziara katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera kwa lengo la kujifunza namna umeme unavyozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa wananchi, Meneja wa Huduma za Usalama wa TANESCO, Bw. Lenin Kiobya, amesema ziara hiyo imewapa watumishi hao uelewa wa namna Shirika linavyotekeleza majukumu yake, kuanzia uzalishaji, usafirishaji hadi usambazaji wa umeme kwa wananchi.
Amebainisha kuwa uelewa huo ni muhimu kwa Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake ya kutafsiri na kusimamia sheria, hususan inaposhughulikia kesi zinazohusiana na miundombinu ya umeme, ili masuala yanayogusa maslahi ya taifa yaweze kupewa uzito unaostahili.
Aidha, amesema kuwa TANESCO itaendelea kujenga ushirikiano na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwenye miundombinu yake, hatua inayolenga kusaidia kupunguza uhalifu na hujuma zinazoweza kuathiri huduma ya umeme nchini.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Fahamu Mtulya, amesema ziara hiyo katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera imewasaidia Majaji na Mahakimu kuelewa kwa kina umuhimu wa kulinda miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya TANESCO.
Amesema kuwa wamebaini kuwa ucheleweshaji wa mashauri yanayohusiana na uwekezaji na miundombinu ya TANESCO unaweza kuwa na gharama kubwa, hivyo wamekubaliana kuyapa kipaumbele mashauri yanayohusu miundombinu hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Pia, amebainisha kuwa uharibifu wa miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya umeme na reli, huhusisha makosa ya uhujumu uchumi yenye adhabu kali, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wa sheria, ikiwemo Bunge, kushirikiana kubaini na kuziba mianya ya kisheria inayoweza kujitokeza.
Aidha, amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya taasisi za umma, ikiwemo ya TANESCO, akieleza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mali za taifa. Amesema Mahakama pia itatumia Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme.
Naye, Kaimu Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera, Mhandisi William Modest, amesema kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati 80 kupitia mashine mbili, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 40. Umeme huo huingizwa kwenye gridi ya taifa kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.
Aidha, ametoa wito kwa Majaji kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na madhara ya kilimo holela kinachoweza kuzuia mtiririko wa maji kuelekea Bwawa la Mtera.
Amebainisha kuwa Kituo cha Mtera kina umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa umeme nchini, huku kikihudumia zaidi ya vijiji 12. Bwawa la Mtera pia lina umuhimu katika shughuli za uvuvi na kilimo, huku Mto Ruaha ukitoa maji kwa skimu mbalimbali za kilimo katika Nyanda za Juu Kusini.


