NA Mwandishi Maalumu RS Arusha 

Mwenyekiti wa Chama cha Pool Table Mkoa wa Arusha, Fadhili Msangi, amesema mashindano ya Pool Table yanafanyika kwa mara ya pili jijini Arusha, huku msimu huu yakikua zaidi na kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Msangi amesema tofauti na msimu wa kwanza uliokuwa na washiriki nane, mwaka huu mashindano yamepanuka na kushirikisha wachezaji kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Rwanda, Msumbiji, Botswana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku baadhi yao wakiwa ni miongoni mwa wachezaji wanaotambulika katika mchezo huo barani Afrika.

Amesema ukuaji wa mashindano hayo umeifanya Arusha kuwa moja ya vituo muhimu vya mchezo wa Pool Table, akibainisha kuwa baadhi ya washiriki wamefunga safari kutoka mbali, ikiwemo Afrika Kusini, kuja Tanzania kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo.

Aidha, Msangi ameishukuru Serikali kwa ushirikiano katika kufanikisha mashindano hayo, huku akiomba wadau zaidi kujitokeza kudhamini na kuwekeza katika mchezo huo, akisema una nafasi ya kutoa fursa kwa vijana na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Kwa upande wa mashabiki, amesema mwitikio umekuwa mkubwa, ambapo wananchi kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Mwanza, Mufindi, Monduli na Karatu wamefika Arusha kufuatilia mashindano hayo.

Msangi pia amempongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, kwa support iliyotolewa kupitia ofisi yake, akisema mchango huo umeendelea kusaidia kukuza mchezo wa Pool Table nchini.