……….
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa imetoa elimu kwa wadau wa Forodha mkoa wa Pwani wakiwemo wawekezaji wa viwanda, mawakala wa forodha na watumishi wa TRA kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Fedha 2026.
Akifungua mafunzo hayo, Meneja wa TRA mkoa wadau Pwani, Bw. Peter Eliyona, amesema mabadiliko hayo ni muhimu kwa kuboresha utendaji kazi na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani, huku akiwataka wawekezaji kutumia fursa za nafuu ya kodi kuongeza uzalishaji na ajira.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Afisa Forodha Mkuu, Bw. Allan Maduhu, ambaye amesema mabadiliko yaliyofanyika pamoja na mambo mengine yamelenga kulinda viwanda vya ndani na kuweka unafuu wa ushuru wa forodha kwa utaratibu wa Duty Remission kwenye malighafi za kuzalisha bidhaa kwa Wazalishaji nchini ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuhamasisha uwekezaji, kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu nchini (Import substitution).
Ameeleza kwamba Serikali imetoa unafuu wa ushuru wa forodha kwenye malighafi za kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni, nguzo za umeme za zege, nyaya za umeme, Misumari na bidhaa za chuma, malighafi za kutengeneza vifungashio vya maboksi, vifungashio vya kuhifadhi chai na kahawa iliyochakatwa, vifungashio vya mbegu za kilimo pamoja na vifungashio vya maziwa.
Naye mwakilishi wa JFAWM Motors, Bi. Farida Ngwekerwa, amepongeza mabadiliko hayo akisema yatasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi.
TRA imewataka watumishi na wawekezaji kuendelea kuzingatia mabadiliko hayo ya sheria kwa lengo la kukuza uzalishaji wa ndani, ajira na kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.

