Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

WATOTO 116,125 wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, walio chini ya umri wa miaka 10 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone ya Polio kwenye maeneo ya mbalimbali ya vijiji na vitongoji vya eneo hilo.

Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, (DMO) Dkt Lengai Mollel amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wenye umri chini ya miaka 10 wanapata chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio.

Dkt Lengai akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika Mji mdogo wa Orkesumet amesema kampeni ya chanjo ya matone ya polio itakafanyika kuanzia Agosti 27, 2026 hadi Agosti 30.

Amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza kinga ya watoto dhidi ya Polio na kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo, ambao unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo ulemavu wa kudumu.

“Mtoto anaweza kupewa chanjo ya matone katika kampeni hii hata kama aliwahi kupata chanjo hapo awali, kwa kuwa chanjo hiyo inaongeza ulinzi dhidi ya Polio na kuimarisha kinga ya jamii,” amesema Dkt Lengai.

Amesema Wilaya ya Simanjiro imejipanga kikamilifu kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa kwa kushirikisha wataalamu wa afya, viongozi wa Serikali za mitaa, wahudumu wa afya na jamii.

Amesema huduma ya chanjo inatolewa nyumba kwa nyumba, sokoni na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu huku akisisitiza umuhimu wa kila mtoto anayestahili kupata chanjo.

“Ewe mzazi, mlezi, usikubali mtoto apate ulemavu kwa kukosa chanjo, hakikisha Agosti 27 hadi 30 Agosti 2026 anapata chanjo, kinga ya mtoto ni jukumu letu sote,” amesema Dkt Lengai.

Amesema ugonjwa wa Polio unaweza kuambukizwa kwa kutozingatia kanuni za usafi, ikiwemo kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa virusi hivyo, amesisitiza umuhimu wa jamii kuzingatia usafi wa mazingira na usafi binafsi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleya Melita Mollel amesema ana uhakika madiwani wa eneo hilo watashiriki suala hilo ili kuhakikisha watoto wote waliolengwa wenye umri wa chini ya miaka 10 wanapatiwa chanjo hiyo.

Kaleya amesema wazazi na walezi wa watoto wanaopaswa kupatiwa chanjo watapatiwa elimu ya kuhakikisha wanaelewa umuhimu wa chanjo hiyo ili watoto wote wanaohusika waipate.