Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeendelea na utekelezaji wa miradi 10 ya maji katika maeneo ya Kata tofauti.

Akisoma taarifa kwa niaba ya meneja wa RUWASA Wilayani Simanjiro, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, mhandisi Wilson Mollel amesema utekelezaji wa miradi hiyo ya maji inaendelea kufanyika.

Mhandisi Mollel ametaja miradi hiyo ni pamoja na miradi wa maji wa Orchoronyori na uchimbaji wa visima katika kijiji cha Namalulu na Okutu.

“Pia upanuzi wa mradi wa maji Naberera kwenda Losokonoi, Lorbene awamu ya pili) na upanuzi wa maji Komolo kwenda Olembole-Lemshuku,” amesema mhandisi Mollel.

Ametaja ujenzi wa mradi mwingine ni wa Losinyai – Einoth, ujenzi wa mradi wa maji Kimotorok (Oltotoi) na ukarabati wa skimu za maji.

“Miradi yote hiyo ipo kwenye hatua tofauti tofauti ya utekelezaji na baadhi imeanza kutoa huduma ya maji kwa jamii,” amesema mhandisi Mollel.

Hata hivyo, amesema RUWASA Simanjiro kwa kushirikiana na vyombo vya watoa huduma ya maji wamefanya matengenezo ya visima vya maji kijiji cha Lerumo kwa kufanya ukaguzi wa jenereta, kufunga na kubadili nyingine.

“Kufanya matengenezo ya jenereta Narakauwo (Noomokon) kufanya matengenezo ya mashine ya maji Kimotorok na kufanya matengenezo ya miundombinu ya maji Londrekes,” amesema mhandisi Mollel.

Amesema wamefanya matengenezo ya mashine ya maji Okutu juu na Orchoronyori katika bomba kuu liliharibiwa na tembo.

“Matengenezo mengine ni miradi ya maji kijiji cha Sukuro, Emboreet kitongoji cha Katika kijiji cha Ngage, Kitiangare, Langai, Ruvu Remit, Okutu, Landanai na Lerumo,” amesema.

Ameeleza kwamba vituo vya kuchotea maji vipo 1,818 kati ya hivyo vinavyofanywa kazi ni 1,783 vya umma ni 412 na vya majumbani ni 1,187.

“Vituo vya taasisi ni 149 pamoja na mbauti (Cattle trough) za mifugo 35 zinazofanya kazi na idadi hii imepungua kutokana na kuondolewa kwa vituo ambavyo havisimamiwi na RUWASA Simanjiro,” amesema mhandisi Mollel.