Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makala ametoa wito kwa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro ,wilaya na maeneo mengine ya hifadhi katika mkoa wa Arusha kujipanga kikamilifu kukarabati miundombinu ya barabara ili ziweze kupitika muda wote ikiwa ni hatua za kukabiliana na mvua za elnino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Septemba, 2026.
Akiongoza kikao cha Kamati ya Usalama kilichoshirikisha mkoa, wilaya za Karatu na Ngorongoro na menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kilichofanyika Ofisi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zilizopo Karatu Mhe. Makala amesema Mkoa wa Arusha unaongoza kupokea idadi kubwa ya Wageni ambapo msimu wa utalii (high season) unaendelea hivyo ni jukumu la kila taasisi kukarabati barabara, madaraja, mifereji na kuwa na njia mbadala ambazo zinawezesha watalii kufika maeneo ya utalii na kutoka kwa wakati.
“Arusha ndio kitovu cha utalii, lazima tujipange kikamilifu wageni hawakwami kwa njia yoyote, kamati za maafa na taasisi zote zishirikiane kuhakikisha watalii wanaoendelea kuja ikiwepo kuhudumia washiriki wa mkutano wa umoja wa Mabunge Duniani utakaofanyika Arusha mwezi oktoba, 2026” Mhe. Makala
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Abdul-Razaq Badru amesema Ngorongoro inaendelea na ujenzi wa barabara kuu ya kutoka geti la Loduare hadi Golini ambapo kipande cha kilomita 29 kutoka Loduare hadi Seneto ujenzi umeanza na ukarabati wa mtandao wa barabara zingine ndani ya hifadhi zinaendelea kufanyika kila siku.

