Vongozi wa Jimbo la Kiembesamaki, Chama cha ACT Wazalendo, wametakiwa kudumisha umoja na mshikamano, wakielezwa kuwa misingi hiyo ni siri ya mafanikio katika uendeshaji wa chama.
Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya ACT Wazalendo, Seif Khamis Mohammed, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kiembesamaki, ambao ni takwa la kikatiba la chama hicho.
Mohammed amesema uimara wa uongozi wowote, hasa wa chama ambacho wananchi wanaamini kuwa ni jukwaa sahihi la kuwakomboa kutokana na dhiki na hali ngumu wanazokabiliana nazo, unategemea viongozi kudumisha umoja na mshikamano.
“Leo tukianza kufarikiana tutawavunja moyo wale ambao wamejenga imani kubwa na ACT Wazalendo kuwa ndio mkombozi wao,” alisema Mohammed.
Aidha, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Taifa amewataka viongozi na wananchi kwa ujumla kuwa na subira na kuendelea kuwaamini viongozi wa juu wa chama katika yale wanayoyapigania.
“Tuwe na subira, tuwaamini viongozi wetu wanafanya kazi nzuri na tutegemee matunda mazuri katika makubaliano yaliyofikiwa,” alisema.
Akisoma ripoti ya utekelezaji wa shughuli za chama, Katibu wa Jimbo hilo, Rashid Kombo Suleiman, alisema mkutano huo ulikuwa halali baada ya kutimiza akidi, ambapo wajumbe 52 kati ya 60 walihudhuria, sawa na asilimia 86.
Katika mkutano huo, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Taifa aliambatana na Katibu wa Mkoa wa Magharibi B, Salim Ali Khamis, pamoja na Mwandishi wa Vikao vya Kitaifa wa chama hicho, Halim Ibrahim Mohamed.

