Na Happy Lazaro, Arusha.
Uongozi wa Trust St. Patrick Schools uliopo Sakina jijini Arusha umesema unaendelea kuweka mkazo katika utoaji wa elimu bora, malezi na maendeleo ya vipaji vya wanafunzi, huku ukieleza kuwa mazingira ya shule hiyo yameandaliwa kumjenga mtoto kitaaluma, kimaadili na kijamii.
Akizungumza wakati wa mahafali ya wanafunzi wa shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo, Mmoja wa wakurugenzi wa shule za  Trust St. Patrick Schools, Mike Patrick Khanya, amesema shule hiyo inatoa elimu kuanzia ngazi ya daycare, shule ya awali, msingi hadi sekondari.
Amesema daycare inahudumia watoto wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka miwili na nusu, huku shule ya awali ikihudumia watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi mitano, na shule ya msingi ikipokea watoto wenye umri wa miaka sita na kuendelea.
Kwa upande wa sekondari, Khanya amesema shule hiyo inatoa elimu ya O-Level kwa wavulana, huku akieleza kuwa msisitizo mkubwa umewekwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata msingi mzuri wa kitaaluma na malezi.
Khanya amesema kuwa, pamoja na elimu ya darasani, shule hiyo imekuwa ikitoa nafasi kwa wanafunzi kuendeleza vipaji vyao katika michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu, volleyball, basketball na kuogelea.
“Mtoto amekuja hapa anafanya football, volleyball, basketball na swimming. Tuna walimu maalum wa kufundisha, ingawa tunazingatia elimu ya darasani zaidi. Ukifanya vizuri darasani, tunaendeleza na kipaji chako,” amesema Khanya.
Amesema mfumo huo unalenga kuhakikisha kuwa kipaji cha mwanafunzi hakizuii maendeleo yake ya kitaaluma, bali elimu na kipaji vinaendelezwa kwa pamoja kulingana na uwezo wa mtoto.
Akizungumzia matokeo ya shule hiyo, Khanya amesema wanafunzi wanaohitimu katika ngazi mbalimbali wamekuwa wakifanya vizuri wanapoendelea na masomo katika shule nyingine, akieleza kuwa hilo ni miongoni mwa viashiria vya ubora wa msingi wa elimu wanaoupata.
Amesema wanafunzi wanaomaliza elimu ya awali wamekuwa wakionyesha uwezo mzuri wanapojiunga na shule nyingine za msingi, huku upande wa darasa la saba nao ukiendelea kufanya vizuri katika mitihani.
“Shule zetu kuanzia shule za awali tumepata sifa nzuri sana kwa sababu watoto wetu wanapotoka pale na kujiunga na shule nyingine, mara zote wanaenda kuwa vinara kwenye zile shule za msingi ambazo wanaenda kujiunga,” amesema Khanya .
Khanya amesema mafanikio hayo yanaenda sambamba na uwepo wa timu ya walimu na watendaji ambao, kwa pamoja, wanazingatia elimu, malezi, maadili na upendo katika kuwalea wanafunzi.
Katika hatua nyingine, amesema shule hiyo imeandaa programu ya Pre-Form One kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba, ambayo itaanza Septemba Mosi na kumalizika Desemba 5.
Ameongeza kuwa, programu hiyo itawahusisha wavulana na wasichana na inalenga kuwaandaa wanafunzi kabla ya kuanza kidato cha kwanza, huku ikijumuisha masomo ya kawaida pamoja na masomo ya ziada kama kompyuta na lugha ya Kichina.
Amesema  kuwa,wanafunzi pia watapata fursa ya kushiriki shughuli na ziara za kielimu nje ya mazingira ya darasa, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kwa maisha ya sekondari.
Khanya amewataka wazazi kuendelea kushirikiana na shule katika kuhakikisha watoto wanapata elimu na malezi yanayowajenga kuwa watu wenye uwezo, nidhamu na maadili mema.
Ameongeza kuwa, Trust St. Patrick Schools itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuendeleza mfumo unaounganisha elimu ya darasani, vipaji, malezi na heshima kwa imani za wanafunzi.