Mwamvua Mwinyi, Pwani

WATOTO 587,509 walio chini ya umri wa miaka 10 mkoani Pwani wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya polio ya matone aina ya nOPV2, katika awamu ya pili itakayoanza Agosti 27 hadi 30, mwaka huu.

Watoto hao ni sehemu ya watoto milioni 6.5 wanaolengwa kupatiwa chanjo nchini, ukiwemo Mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari na timu ya kampeni ya chanjo kutoka mkoani Pwani na Wizara ya Afya, Agosti 22, 2026, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Pwani, Alfred Ngoi, amesema mkoa umejiandaa kikamilifu kwa kampeni hiyo, huku vifaa vikiwa tayari na watoa huduma mbalimbali kupewa mafunzo.

Ngoi ameeleza ugonjwa wa polio unasababishwa na virusi vinavyoweza kumfanya mtoto kupooza na hata kupoteza maisha, huku akisisitiza kuwa ugonjwa huo hauna tiba, bali unazuilika kwa chanjo.

“Chanjo ya nOPV2 ni salama na hutolewa mahsusi kupitia kampeni za chanjo ili kuzuia maambukizi ya polio, na kwamba haitumiki kama sehemu ya ratiba ya kawaida ya chanjo.”

Kwa mujibu wa Ngoi, chanjo hiyo itatolewa nyumba kwa nyumba, katika vituo vya kutolea huduma za afya, zahanati na hospitali, pamoja na shuleni na maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama masoko, stendi na nyumba za ibada.

Kwa upande wake, Ofisa kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Kinga na Chanjo, Flora Kazoba, aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa wa polio unaoweza kusababisha ulemavu.

Kazoba amesema awamu ya kwanza ya kampeni hiyo ilifanyika kati ya Machi na Mei katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amefafanua kuwa awamu ya pili itahusisha mikoa nane ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma na Mara, huku awamu ya tatu ikitarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2, mwaka huu katika mikoa sita.

Vilevile, Kazoba amefafanua Wizara ya Afya inaendelea na mkakati wa kukabiliana na ugonjwa wa polio kwa kufanya uchunguzi wa kupima maji taka ili kubaini uwepo wa virusi vya polio na kuzuia kuenea kwa maambukizi.

Anasema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa virusi vya polio vinaweza kuenea kupitia mazingira ya maji taka na maeneo yenye maji yaliyotuama, ambako watoto wanaweza kucheza na kuathirika.