WATAALAMU wa kada ya ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi wametakiwa kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakiweka usalama, afya na maslahi ya umma mbele katika maamuzi yao ya kitaaluma.
Rai hiyo imetolewa leo Agosti 21, 2026, na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Elias Kissamo, katika Sherehe ya Tatu ya Uthibitisho wa Kitaaluma ya AQRB iliyowahusisha wataalamu kutoka kada mbalimbali.
Kissamo amesema sherehe hiyo si ya kupokea vyeti pekee, bali ni uthibitisho kwamba wataalamu hao wamefikia viwango vya maarifa, uwezo, uzoefu na mwenendo vinavyohitajika kwa mtaalamu aliyesajiliwa, hivyo usajili wa kitaaluma ni dhamana kwa umma.
“Msiruhusu fedha, maslahi binafsi, shinikizo la mteja au mwajiri kuathiri maamuzi yenu ya kitaaluma,” amesema
Kissamo, huku akiwataka wataalamu hao kutosaini wala kuthibitisha kazi ambayo hawajaipitia na kujiridhisha nayo kitaaluma.
Amesema wataalamu hao wanaingia rasmi katika taaluma wakati Tanzania ikielekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayohitaji miji bora, makazi salama, miundombinu yenye ubora, uwekezaji wenye tija, matumizi bora ya rasilimali na mazingira yaliyojengwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Makamu Mwenyekiti huyo pia amewataka wataalamu kujiandaa na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kubadilisha sekta ya ujenzi, ikiwemo matumizi ya Building Information Modelling (BIM), Akili Bandia (AI), usimamizi wa miradi kidijitali na majengo janja.
Amesema teknolojia inapaswa kutumika kuongeza ubunifu, tija na ushindani wa wataalamu, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya uwajibikaji wa kitaalamu, akisisitiza kuwa teknolojia inaweza kusaidia uamuzi wa kitaaluma lakini haiwezi kuchukua nafasi ya uwajibikaji wa mtaalamu.
Awali, akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Penina Mabonye amesema wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji, huku wakizingatia usalama, afya na maslahi ya umma katika huduma zao za kitaaluma.
Amesema usajili huo si tu utambuzi wa mafanikio yao ya kitaaluma, bali ni dhamana kubwa waliyopewa na jamii na Taifa katika masuala yanayohusu majengo, miundombinu, gharama za miradi, usimamizi wa miradi na maeneo mengine yanayohusiana na taaluma zao
.
Aidha, Mabonye amesema watazingatia sheria, kanuni, By-Laws na Kanuni za Maadili zinazosimamia taaluma zao, huku wakiepuka kutumia taaluma kwa maslahi binafsi yanayoweza kuathiri haki, ubora au uaminifu wa kazi zao.
Amesema wataalamu hao wataendelea kutoa huduma zinazozingatia thamani ya fedha, ubora, usalama na maendeleo endelevu, kwa kuzingatia wajibu wao kwa jamii na Taifa.
Mabonye ameishukuru Bodi ya AQRB kwa kusimamia taaluma zao, kuweka na kulinda viwango vya kitaaluma na kuhakikisha mchakato wa usajili unajenga uwezo, nidhamu, uwajibikaji na uadilifu unaohitajika katika kuhudumia jamii.

