Mhariri Mkuu wa maudhui mtandaoni wa Fullshangwe Blog, John Bukuku, ametwaa tuzo ya ushindi wa kwanza katika kundi la vyombo vya habari vya kidijitali kwa uandishi wa habari unaohusu dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Bukuku amepata ushindi huo katika hafla iliyofanyika mjini Babati, mkoani Manyara, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikisha wahariri na waandishi wa habari kutoka Kanda ya Kaskazini.
Kikao hicho kiliwakutanisha wadau wa habari kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, ambapo pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya TMDA na vyombo vya habari, washiriki walipata fursa ya kutambua na kuenzi kazi bora za uandishi wa habari katika sekta ya dawa na vifaa tiba.
Katika tuzo hizo, Bukuku alitangazwa mshindi wa kwanza katika kipengele cha Digital, na kukabidhiwa cheti cha ushindi, ngao pamoja na zawadi ya fedha taslimu.
Kwa upande mwingine, washindi katika makundi mengine walijumuisha Aveline Kitomari wa Habari Leo na Daily News aliyeshinda kipengele cha Magazeti, huku Taus Mbowe wa Star TV akitwaa ushindi katika kipengele cha Televisheni.
Agatha Kisimba wa Radio Maria naye alifanikiwa kuibuka mshindi katika kipengele cha Radio, na kufanya waandishi hao kutoka majukwaa mbalimbali kutambuliwa kwa mchango wao katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.


