NA DENIS MLOWE ,IRINGA 

WAKULIMA wameeleza namna matumizi ya mbegu bora yanavyoweza kubadili matokeo ya kilimo, wakisisitiza umuhimu wa kupata mbegu zinazofaa kwa mazingira ya eneo husika na kufuata ushauri wa wataalamu kabla ya kuanza msimu wa kilimo.

Agustino Sanga, mkulima wa mpunga kutoka Pawaga, amesema matumizi ya mbegu bora yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mpunga, huku akiwataka wakulima wenzake kuachana na tabia ya kutumia mbegu bila kujua ubora na sifa zake.

Amesema mkulima anapaswa kufahamu aina ya mbegu anayopanda, muda sahihi wa kupanda pamoja na mahitaji mengine muhimu ya zao ili kupata matokeo mazuri wakati wa mavuno.

Kwa upande wake, Miriam Ahmed, mkulima kutoka Wilaya ya Kilolo, amesema upatikanaji wa mbegu bora ni jambo muhimu kwa mkulima anayelenga kuongeza uzalishaji na kipato kupitia kilimo.

Amesema wakulima wanahitaji elimu zaidi kuhusu uchaguzi na matumizi ya mbegu, kwani mbegu bora zinapaswa kuambatana na maandalizi mazuri ya shamba na matumizi sahihi ya pembejeo nyingine.

Wakulima hao wameeleza hayo wakati wakizungumzia umuhimu wa matumizi ya mbegu zinazozalishwa na Agricultural Seed Agency (ASA), Wakala wa Mbegu za Kilimo wa Serikali, ambao unahusika na uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kuongeza tija.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Mgongolwa Agrovet and Seed Company Limited, Joseph Mgongolwa, amesema wakulima wanapaswa kuiona mbegu bora kama msingi wa safari ya uzalishaji, badala ya kuichukulia kama pembejeo nyingine ya kawaida.

Amesema ASA imekuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, huku akiwataka kutumia mbegu hizo kwa kuzingatia maelekezo na ushauri wa wataalamu.

“Tunachotaka mkulima akielewe ni kwamba mbegu ndiyo mwanzo wa mavuno ukianza na mbegu sahihi, ukaandaa shamba vizuri, ukatumia mbolea kwa usahihi na ukafuatilia zao lako, unaongeza uwezekano wa kupata uzalishaji mzuri,” amesema Mgongolwa.

Aidha, amesema wakulima wanapaswa kuchagua mbegu kwa kuzingatia aina ya zao, mazingira ya eneo lao na malengo ya uzalishaji, badala ya kuchagua kwa mazoea au kwa kuangalia bei pekee.

Mgongolwa amesema kampuni yake itaendelea kuwa karibu na wakulima kwa kuwapatia mbegu pamoja na elimu ya matumizi yake, akisisitiza kuwa lengo ni kuona mkulima anapata tija zaidi na hatimaye kuongeza kipato kupitia kilimo.

Amesema kilimo cha kisasa kinahitaji mkulima kufanya maamuzi sahihi tangu hatua ya kuchagua mbegu hadi wakati wa kuvuna, ili kila msimu uwe fursa ya kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha.