Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Denis Simba, amesema matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NeST) yamewezesha kuzuia uchapishaji wa zaidi ya karatasi milioni 288.6 za nyaraka za zabuni, hatua iliyookoa takribani Shilingi bilioni 27.64.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Agosti 20, 2026 kuhusu utekelezaji wa PPRA kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka 2026/27,amesema kuwa matumizi ya NeST yamepunguza gharama na muda kwa wazabuni wanaoshiriki katika michakato ya ununuzi wa umma.
Amesema kabla ya matumizi ya mfumo huo, wazabuni walilazimika kuchapisha na kusafirisha nyaraka za zabuni kwenda kwenye ofisi za ununuzi, lakini NeST imeondoa ulazima huo kwa kuwezesha michakato kufanyika kwa njia ya kielektroniki.
“Matumizi ya mfumo wa NeST yamewezesha kuzuia uchapishaji wa zaidi ya karatasi milioni 288.6 za nyaraka za zabuni, sawa na kuokoa takribani Shilingi bilioni 27.64,” amesema Bw. Simba.
Amesema mfumo huo pia umewezesha wazabuni kuomba zabuni wakiwa mahali popote kupitia vifaa vya kidijitali, ikiwemo simu janja, na kupata taarifa za zabuni kupitia mfumo huo bila kulazimika kufika kwenye ofisi za taasisi nunuzi.
Huku akibainisha Kuwa NeST imeendelea kuboresha uwazi na ufanisi katika ununuzi wa umma, huku mfumo huo ukiwa umeunganishwa na zaidi ya mifumo 30, ikiwemo ya benki, malipo, Hifadhi ya Jamii, bodi za usajili wa wataalamu na mifumo ya leseni.
Amesema matumizi ya NeST pia yameongeza uzingatiaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma kutoka asilimia 65 mwaka 2023/24 hadi asilimia 76 mwaka 2024/25 na kufikia asilimia 79 mwaka 2025/26.
Aidha, amebainisha Kuwa NeST umewezesha utekelezaji wa upendeleo kwa wazabuni wazawa, ambapo zabuni zenye thamani isiyozidi Shilingi bilioni 50 zimetengwa kwa wazabuni wazawa pekee, huku wazabuni wa ndani wakipewa upendeleo wa hadi asilimia 10 katika zabuni zenye ushindani wa kimataifa.
Aidha, amesema makundi 27,996 maalum yamesajiliwa kwenye NeST, yakiwemo makundi 13,317 ya vijana, 14,400 ya wanawake, 643 ya wazee na 586 ya watu wenye ulemavu, huku yakipata zabuni zenye jumla ya thamani ya Shilingi bilioni 56.
Amesema PPRA inalenga kufikisha idadi ya makundi maalum yaliyo tayari kushiriki zabuni hadi laki tatu ifikapo mwaka 2050, hatua inayolenga kuongeza fursa za ajira na ushiriki wa Watanzania katika uchumi kupitia ununuzi wa umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kazi iendelee Group, Elizabeth Kasinga, amesema kundi hilo limefanikiwa kupata zabuni 21 zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.1966 kutoka katika Wizara mbalimbali za Serikali na kuwezesha zaidi ya vijana 450 kupata ajira, akiwataka Watanzania kutumia fursa zinazotolewa kupitia mfumo wa NeST.

