Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na vyombo vya habari katika kulinda afya ya jamii.

Bi. Sendiga amesema hayo wakati akifungua kikao cha siku mbili kati ya TMDA, wahariri na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya TMDA, udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na changamoto zinazojitokeza katika eneo hilo.

Amesema taarifa sahihi kuhusu bidhaa za tiba ni muhimu kwa sababu sekta hiyo inahusisha moja kwa moja afya na mustakabali wa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili waweze kufanya maamuzi salama kuhusu matumizi ya dawa na vifaa tiba.

“Tunapozungumzia bidhaa za tiba tunazungumzia afya na mustakabali wa jamii yetu kwa ujumla. Hivyo ni muhimu wananchi wapate taarifa sahihi kuhusu dawa, vifaa tiba na namna ya kutambua bidhaa zinazokidhi viwango,” amesema Bi. Sendiga.

Amesema TMDA ina jukumu muhimu la kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyowafikia wananchi vinakuwa na ubora, usalama na ufanisi, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa jukumu hilo unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, hususan vyombo vya habari ambavyo vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo wa TMDA, Dkt. Yona H. Mwalwisi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, inayoiwezesha kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.

Dkt. Mwalwisi amesema TMDA imejenga utamaduni wa kukutana na wahariri na waandishi wa habari kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini ili kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuboresha udhibiti wa bidhaa za tiba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Amesema utafiti wa kuridhika kwa wananchi na wateja uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hususan Shule ya Biashara, mwezi Desemba 2022 katika halmashauri 35 za mikoa 16, umeonesha kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu TMDA kutoka asilimia 47 mwaka 2020, huku kiwango cha kuridhika na huduma za mamlaka hiyo kikiwa asilimia 82.

Dkt. Mwalwisi amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano kati ya TMDA na vyombo vya habari, ambavyo vimekuwa daraja muhimu la kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba, pamoja na kuwaelimisha kuhusu hatari za bidhaa bandia, duni na zisizosajiliwa.

Aidha, amesema TMDA imeendelea kushikilia cheti cha mfumo wa usimamizi wa ubora ISO 9001:2015 pamoja na ithibati ya maabara kwa kiwango cha ISO 17025:2017, jambo linalothibitisha kuwa mifumo na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo zinakidhi viwango vya kimataifa.

Amesema TMDA pia imetambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa mamlaka iliyofikia ngazi ya tatu ya ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa bidhaa za tiba, huku ikiendelea na juhudi za kufikia ngazi ya nne, ambayo ndiyo ya juu zaidi, na kuendelea kuwa miongoni mwa mamlaka zinazoongoza barani Afrika.

Dkt. Mwalwisi amesema mamlaka hiyo imeimarisha ufuatiliaji wa usalama wa dawa na chanjo baada ya kuingia sokoni, ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kufuatilia madhara ya dawa na chanjo hadi kufikia vituo 33 nchini, huku mtandao wa maabara hamishika ukiongezeka kutoka 19 hadi 28, hatua inayowezesha upimaji wa sampuli katika maeneo mbalimbali kwa wakati.

Amesema TMDA pia imeweka vituo vya maabara katika vituo vyote 16 rasmi vya forodha vinavyoingiza bidhaa za tiba nchini, hatua inayolenga kuhakikisha ubora wa dawa unapimwa kabla bidhaa hizo hazijaingia katika soko la Tanzania. Aidha, mamlaka hiyo imekamilisha ujenzi wa tanuru la kisasa jijini Dodoma kwa ajili ya kuteketeza bidhaa za tiba zilizo duni, bandia, zilizokwisha muda wa matumizi na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.

Dkt. Mwalwisi amesema kikao hicho pia kinalenga kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, mikakati ya TMDA katika kupambana na bidhaa bandia, duni na zisizosajiliwa, pamoja na kuwafahamisha kuhusu fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa za tiba nchini ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.