NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Benjamini Sitta, amewataka madiwani wa Manispaa ya Iringa kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri ili kuiwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Sitta alitoa wito huo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Iringa, ambapo alisema ongezeko la mapato litasaidia kupunguza changamoto za kifedha na kuwezesha halmashauri kutekeleza mipango yake kwa ufanisi.
Alisema madiwani wana nafasi kubwa ya kusaidia halmashauri kuongeza mapato kwa kushirikiana na watendaji na kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazotakiwa kisheria.
“Tuendelee sana kupambana namna gani ya kupata mapato najua mnapokuwa na mapato, hata mvutano wa hizi bajeti ndogo ndogo unapungua,” alisema Sitta.
Aliwapongeza madiwani kwa namna wanavyoshiriki katika mijadala ya baraza, akisema kuhoji na kutaka ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ni sehemu ya uwajibikaji kwa wananchi waliowachagua.
Alisema baraza la madiwani halipaswi kuwa la kupitisha kila jambo bila mjadala, bali madiwani wanapaswa kuhoji na kuhakikisha maamuzi yanayofanyika yanazingatia maslahi ya wananchi na maendeleo ya Manispaa.
“Watu wanahoji, watu wanataka ufafanuzi. Kama baraza lingekuwa la rubber stamp, watu wanagonga meza tu, mnakuwa hamtendei haki wale wananchi waliowachagua,” alisema.
Sitta pia aliipongeza Manispaa ya Iringa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akisema ziara alizofanya katika maeneo mbalimbali zimemuwezesha kuona maendeleo katika miradi ya shule, zahanati na miundombinu ya barabara.
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa TACTIC, alisema Manispaa imenufaika na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 5.6, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa hiyo.
Aidha, aliwataka madiwani kushirikiana na watendaji kuhakikisha maeneo yanayopitiwa na barabara mpya, ikiwemo barabara za bypass, yanapimwa mapema ili kuzuia migogoro ya ardhi na makazi holela.
Alisema ujenzi wa barabara mpya huongeza thamani ya ardhi katika maeneo husika, hivyo ni muhimu hatua za upimaji kuchukuliwa mapema kabla ya kuibuka kwa migogoro ya umiliki.
“Maeneo haya yanaenda kupanda thamani. Kama hatujayapima, tunaenda kutengeneza migogoro mikubwa sana,” alisema.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alisema halmashauri inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa ofisi mpya ya halmashauri katika eneo la Kisa Kilolo, mradi unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni nne.
Alisema pia miradi ya Soko la Kihesa, Ofisi ya Wahandisi, barabara katika maeneo ya Mkimbizi na Mtwivila inaendelea kutekelezwa.
Meya alisema ukarabati huo awali ulikadiriwa kugharimu shilingi milioni 70, lakini hadi sasa umetumia takribani shilingi milioni 36, na baada ya kujumlisha VAT gharama imefikia karibu shilingi milioni 45.
Alisema Machinjio ya Kisasa ya Ngelewala yanatarajiwa kuanza kufanya kazi baada ya kukamilika kwa ufungaji wa mtambo huo, hatua ambayo itaongeza uwezo wa Manispaa katika huduma za uchinjaji na uhifadhi wa nyama.

