Na John Walter -Babati
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka mkazo katika kuzuia ugonjwa wa kupooza (Polio) kwa kuendesha kampeni maalum ya chanjo itakayowafikia watoto zaidi ya milioni 6.5 katika mikoa nane nchini.
Kampeni hiyo inatarajiwa kufanyika Agosti 27 hadi 30, 2026, ambapo chanjo itatolewa nyumba kwa nyumba bila malipo, huku watoto wakichanjwa bila kujali kama waliwahi kupata chanjo katika awamu zilizopita.
Hatua hiyo imekuja baada ya ufuatiliaji wa kitaalamu kubaini uwepo wa virusi vya Polio kwenye maji taka yenye kinyesi mwaka 2025 na mwanzoni mwa mwaka 2026 katika Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya uhamasishaji wa huduma za chanjo kwa waandishi wa habari yaliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Komoto mjini Babati, Meneja wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Georgina Joachim, amesema ugonjwa wa Polio ni hatari na ndiyo sababu Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha kinga dhidi yake.
Dkt. Joachim, pamoja na Dkt. Christopher Bulula, wameeleza kuwa lengo la Wizara ni kuhakikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa chanjo na changamoto ya Polio unawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.
Kampeni hiyo itatekelezwa katika mikoa nane ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Dodoma na Mara, ambapo jumla ya watoto 6,555,511 wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kupata chanjo.
Kwa upande wa Mkoa wa Manyara, jumla ya watoto 675,630 wanatarajiwa kufikiwa na chanjo hiyo.
Wataalamu wa afya wameeleza kuwa Polio haina tiba, lakini ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa chanjo inayotolewa kwa njia ya matone, ikiwemo chanjo ya nOPV2.
Wamewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo kwa wakati na kuwapeleka kliniki mara kwa mara ili kupata huduma muhimu za afya.
Kwa sasa, hakuna mtoto aliyethibitika kuugua Polio nchini Tanzania, huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kinga ili kuzuia ugonjwa huo kuingia au kusambaa nchini.
Mafunzo kwa Waandishi wa Habari
Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yamefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kampeni hiyo, yakilenga kuwapa wataalamu wa habari uelewa sahihi kuhusu Polio, umuhimu wa chanjo na namna ya kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa usahihi.
Waandishi wa habari wametakiwa kutumia nafasi yao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto kupata chanjo na kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kampeni ya nyumba kwa nyumba inafikia watoto wote wanaolengwa.
Kampeni ya chanjo ya Polio itaanza rasmi Agosti 27 na kumalizika Agosti 30, 2026, na huduma hiyo itatolewa bure kwa watoto wanaolengwa.

