Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaofanyika Agosti 22, mwaka huu, wilayani Rufiji, ni hatua kubwa ya kihistoria katika kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini, kuchochea sekta ya viwanda na kukuza uchumi.
Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, unaotekelezwa kwa asilimia 60 katika Mkoa wa Pwani na asilimia 40 katika Mkoa wa Morogoro, unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya kuchochea shughuli za uzalishaji na kuwa chachu ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Agosti 20, 2026, Kunenge alisema Mkoa wa Pwani unajivunia kuwa mwenyeji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati, huku akieleza kuwa uzalishaji wa umeme huo utaongeza nguvu katika Gridi ya Taifa na kusaidia kukidhi mahitaji ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa katika Awamu ya Tano ya Serikali, huku Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiupokea na kuuendeleza ukiwa umefikia zaidi ya asilimia 30 ya utekelezaji, hatua aliyowezesha kutimizwa kwa ndoto ya mwanzilishi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“JNHPP ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ya nishati nchini, ukitarajiwa kusafirisha umeme kupitia njia mbalimbali za Gridi ya Taifa na vituo vya kupozea umeme vya Chalinze–Kinyerezi, Kwala–Zegereni–Zinga na Dundani–Msufini Mkuranga,” alisema. Kunenge.
Kunenge alisema tija ya mradi huo imeanza kuonekana, kwani umeongezeka kutoka megawati 118 mwaka 2022 hadi megawati 356 kufikia Julai 2026.
“Tija imeshaanza kuonekana kwani mwaka 2022 tulikuwa tunapata umeme megawati 118, hadi kufikia Julai 2026 tumefikia megawati 356 kutoka katika bwawa hilo kuzalisha umeme unaoingia katika Gridi ya Taifa,” alifafanua Kunenge.
Vilevile, Kunenge alisema sekta ya viwanda na uwekezaji imeendelea kukua kwa kasi katika Mkoa wa Pwani, huku mkoa ukiwa na jumla ya viwanda vikubwa na vya kati 495.
Alisema katika kipindi cha Awamu ya Sita tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, viwanda vipya 307 vimeanzishwa, akieleza kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme na gesi umechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia uwekezaji huo.
Kuhusu uhifadhi wa vyanzo vya maji, Kunenge aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na kulinda mazingira yanayozunguka bwawa hilo, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha uzalishaji wa umeme unaendelea kuwa endelevu.
Alieleza kuwa, sambamba na matumizi ya maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, Serikali inapanga kujenga bwawa la maji safi litakalotumika kwa matumizi ya wananchi wa Pwani na Morogoro, huku mpango huo ukitarajiwa kunufaisha hadi Mkoa wa Lindi.
Kunenge alisema Serikali pia inaanzisha mfumo wa Gridi ya Maji utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha na kusambaza takribani lita za ujazo milioni 1.5 za maji kwa siku, ambapo kwa kuanzia uzalishaji utakuwa lita 750,000 .
Hata hivyo, Kunenge alisema Mkoa wa Pwani uko salama na umejipanga kikamilifu kuhakikisha uzinduzi huo unafanyika kwa mafanikio.
Alibainisha Serikali inaendelea na jitihada za kuwekeza katika nishati ya umeme, huku akibainisha kuwa kwa sasa inaendelea na hatua za kukamilisha mradi wa gesi kutoka Kinyerezi kwenda Chalinze.
Pia Kunenge alieleza ,vijiji vya Mkoa wa Pwani vinaendelea kunufaika na upatikanaji wa umeme, huku vijiji vinane vilivyopo visiwani vikitarajiwa kupata umeme kupitia nishati ya jua na vitongoji 1,220 sawa na asilimia 65 vimefikiwa na huduma ya umeme.

