Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Maguha Stephano akitoa elimu ya magonjwa ya saratani na yasiyo ya kuambukiza kwa watumishi wa Wizara ya Fedha wakati wa zoezi la upimaji afya linalofanyika kwa watumishi hao waliopo Treasury Square jijini Dodoma.
Na Mwandishi Maalumu – Dodoma
19/08/2026 Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza ili kubaini hali zao za kiafya mapema na kuchukua hatua stahiki kabla magonjwa hayo hayajawa makubwa.
Rai hiyo imetolewa jana na Kamishna Msaidizi wa Uchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha, William Muhoja wakati wa utoaji wa elimu ya saratani na magonjwa yasiyoambukiza iliyotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kabla ya kuanza kwa zoezi la uchunguzi wa afya kwa watumishi wa wizara hiyo waliopo katika jengo la Treasury Square jijini Dodoma.
Muhoja alisema watumishi wamefurahishwa na kupata huduma pamoja na elimu waliyopewa na wataalamu wa ORCI huku akibainisha kuwa elimu hiyo imewasaidia kuondoa hofu iliyokuwepo miongoni mwao kuhusu vipimo vya saratani.
Alisema semina hiyo imekuwa muhimu kwa kuwa imewapa watumishi uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya afya ambayo awali hawakuwa na taarifa zake huku pia wakiandaliwa kisaikolojia kabla ya kufanyiwa vipimo.
“Semina ni nzuri kwa sababu kuna vitu ambavyo hatukuwa tunavijua lakini baada ya semina tumepata uelewa. Pia tumeandaliwa kisaikolojia hivyo imetusaidia kuondoa hofu ya kupima”, alisema Muhoja.
Muhoja alisema wamegundua kuwa vipimo vya saratani hususan vya tezi dume kwa wanaume ni rahisi kuliko walivyokuwa wakidhani kutokana na taarifa walizokuwa wakisikia awali kuwa vilikuwa siyo rafiki na hivyo kuwafanya wengi kuogopa kupima.
Alisema elimu hiyo imewasaidia watumishi kuelewa umuhimu wa kupima na kuchukua hatua mapema huku baadhi yao wakipatiwa huduma nyingine za afya ikiwemo chanjo ya homa ya Ini.
“Vipimo ni rahisi hasa vipimo vya saratani kwa wanaume kwani tumefanya kwa njia ya damu, ultrasound, choo na mkojo tofauti na tulivyokuwa tunasikia. Kwa hiyo ni muhimu watu wasiwe na hofu ya kupima wajitokeze kupima”, alisema.
Kwa upande wao watumishi wa Wizara ya Fedha waliishukuru ORCI kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali ya afya zao na kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza.
Mmoja wa watumishi hao Eva Masasi ambaye alipata nafasi ya kupima saratani za magonjwa mbalimbali zikiwemo za matiti na shingo ya kizazi aliwahimiza wafanyakazi wengine kutumia fursa zinazotolewa na wataalamu wa afya na kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.
Alisema watumishi hawapaswi kusubiri hadi tatizo liwe kubwa ndipo waanze kutafuta matibabu bali wanapaswa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kufahamu hali zao na kuchukua hatua mapema.
“Wasiogope kupima kwa sababu tiba ipo. Tunapaswa kujenga utaratibu wa kupima afya zetu mara kwa mara badala ya kusubiri tatizo liwe kubwa ndipo tuanze kuhangaika na matibabu”, alisema Masasi.
Naye Paul Mfilinge Mtumishi wa Wizara hiyo aliwahimiza watumishi wenzake kutumia fursa hiyo kupima afya kwa kuwa si kila wakati hupatikana nafasi ya kupata elimu na huduma za uchunguzi wa afya mahali pa kazi.
Alisema elimu ya saratani na magonjwa yasiyo ya kuambukiza imekuwa na manufaa makubwa kwa watumishi kwa kuwa imewapa elimu kuhusu mambo ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu huku vipimo vikiwasaidia kujua hali zao za kiafya.
Zoezi hilo limekuwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha watumishi kujenga utamaduni wa uchunguzi wa afya zao mara kwa mara hatua inayoweza kusaidia kugundua magonjwa mapema na kuchangia afya bora pamoja na tija katika utendaji wa kazi.
Watumishi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) wakimsikiliza Mkurugenzi wa Kinga wa Taasisi hiyo Dkt. Crispin Kahesa wakati akitoa elimu ya magonjwa ya Saratani kwa watumishi wa Wizara ya Fedha wakati wa zoezi la upimaji afya linalofanyika kwa watumishi hao waliopo Treasury Square jijini Dodoma.
Watumishi wa Wizara ya Fedha wakimsikiza Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Frank Rutachunzibwa wakati akitoa elimu ya magonjwa ya saratani kwenye zoezi la upimaji afya linalofanyika kwa wafanyakazi hao waliopo Treasury Square jijini Dodoma.
(Picha na ORCI)
