Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya), Mhe. Dkt. Jafar Seif, amesema ugatuzi wa madaraka ni msingi wa kufanikisha Dira ya Taifa 2050, akisisitiza kuimarishwa kwa Serikali za Mitaa ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.Ameyasema hayo Jijini Dodoma, Agosti 19, 2026, wakati akifungua Mkutano wa 16 wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA), akimwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe. Amesema ugatuzi wa madaraka unawapa wananchi nafasi ya kushiriki katika maamuzi na maendeleo yanayowahusu.

Mhe. Dkt. Seif amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kiutendaji na usimamizi wa fedha, ikiwemo kupeleka fedha za miradi ya maendeleo moja kwa moja katika taasisi za Serikali za ngazi za chini, zikiwemo shule, zahanati, ofisi za kata na vijiji.

Amesema kufikia Dira ya Taifa 2050 kunahitaji Serikali za Mitaa zenye uongozi bora na uwajibikaji, mipango madhubuti ya maendeleo, usimamizi mzuri wa rasilimali za umma na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto ya umeme, huku akieleza kuwa upatikanaji wa umeme utawezesha wananchi kuongeza uzalishaji, kuanzisha viwanda na kufanya biashara, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.

Amewataka wataalamu wa Serikali za Mitaa kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuwekeza katika miradi yenye tija, kutoa huduma bora na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa usahihi. Amesema mafanikio ya ugatuzi yanategemea uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi.

Mhe. Dkt. Seif ameitaka TOA kuendelea kuwa jukwaa la wataalamu na viongozi wa Serikali za Mitaa katika kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto za wananchi. Pia amewataka viongozi na watendaji kutafsiri kwa vitendo kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu kwa Watanzania kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Amesisitiza kuwa ugatuzi wa madaraka ni nguzo ya Dira ya Taifa 2050, hivyo viongozi, watendaji, wadau wa maendeleo na wananchi wanapaswa kushirikiana kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma ili kujenga Tanzania yenye uchumi imara na huduma bora za kijamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TOA, Bw. Albert Msovela, amesema taasisi hiyo inawajumuisha Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wanachama na kuishauri Serikali kuhusu maendeleo ya Serikali za Mitaa na ugatuaji wa madaraka (D by D).

Amesema TOA itaendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha utawala bora, utoaji wa huduma kwa wananchi na usimamizi wa rasilimali, huku ikihamasisha ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya maendeleo. Amesema mkutano mkuu wa 16 wa TOA wa mwaka 2026 unaongozwa na kaulimbiu inayosisitiza ugatuaji wa madaraka katika Serikali za Mitaa kuwa msingi wa kufikia Dira ya Taifa 2050.

Pia amesema Kuwa TOA itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato, utoaji wa huduma bora, usimamizi wa mazingira na kuimarisha Serikali za Mitaa. Pia amewashukuru wadhamini waliofanikisha mkutano huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.