Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Ilala imefanya kikao na Washauri wa Kodi ambapo pande hizo mbili zimeeleza azma ya kuendelea kushirikiana katika kuwaelimisha walipakodi haki na wajibu wao.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 18 Agosti, 2026, jijini Dar es Salaam, Meneja TRA Ilala Bw. Musibu Shabani amesema kuwa TRA inatambua nafasi ya washauri wa kodi katika kuwasaidia wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kikodi.

Aidha amewasisitiza kuendelea kushirikiana na TRA katika kuwajengea walipakodi uelewa wa haki walizonazo pamoja na wajibu wao wa kikodi.

“Mbali na kuwa wateja wenu, wafanyabiashara pia ni walipakodi wanaotegemewa katika kuijenga nchi. Kama wataalamu, tunapaswa kushirikiana katika kuwawezesha kutimiza wajibu wao ili ulipaji wa kodi usiwe mzigo kwao,” amesema Shabani.

Ameongeza kuwa milango ya TRA iko wazi katika kuhakikisha changamoto zote za kikodi zinazowakumba washauri wa kodi na wateja wao zinatatuliwa na kuwaahidi huduma bora.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania (TATC) Bw. Sospeter Kibishi ameahidi kwa niaba ya washauri hao kuwa wataendelea kushirikiana na TRA kutoa elimu na kuimarisha uhusiano ili kuweka mazingira mazuri ya ulipaji wa kodi nchini