Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wakulima kujiandaa mapema na msimu wa mvua za Vuli 2026, huku ikitabiri mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini.
Mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, kuanzia Oktoba hadi Desemba 2026, huku baadhi ya maeneo yakianza kupata mvua hizo mapema kuanzia wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa (IPCC), Dkt. Ladislaus Benedict Chang’a, amesema maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Amesema mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara, inayozunguka Ukanda wa Ziwa Victoria, nayo inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kutokana na mwelekeo huo, Dkt. Chang’a amewataka wakulima kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa katika kupanga shughuli zao za kilimo, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kilimo, kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua pamoja na kuchukua hatua za kudhibiti visumbufu vya mimea.
Amesema hatua hizo zitasaidia kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mwenendo wa mvua, ikiwemo magonjwa ya mimea, na kuongeza uzalishaji wa mazao.
TMA imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua kadri zitakavyohitajika, huku ikiwasihi wadau kutoka sekta mbalimbali kuwasiliana na Mamlaka kwa ajili ya kupata utabiri mahsusi unaoendana na mahitaji ya sekta zao.

